Bw. Nairoti Kenanda kutoka kijiji
cha Njoroi katika tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha
akishiriki kuchimba shimo lenye urefu wa mita moja kwa ajili ya kuwekwa
alama ndogo ya mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya unaopita
katika kijiji hiko.
Wanakijiji wa Kijiji cha Sukenya
katika kata ya Soitsambu wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakisoma
vipeperushi walivyopewa wakati wa utoaji elimu na uhamasishaji kuhusu
uimarishaji wa mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya ulioanza
mkoani Arusha.
……………..
Na Rehema Isango, Arusha
Jumla ya kilomita 91 za mpaka wa
Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya mkoani Mara zimeimarishwa na sasa
timu za wataalam wa upimaji ardhi na ramani zimeanza kazi hiyo wilayani
Ngorongoro katika mkoa wa Arusha.
Kiongozi wa timu ya wataalam
kutoka Tanzania Bw. Isaack Marwa amefafanua kuwa jumla ya alama kuu 66
zenye umbile la pembetatu zimeimarishwa ambapo kati ya hizo, 47
zimejengwa upya baada ya kung’olewa na 19 zimekarabatiwa baada ya
kuchakaa katika maeneo ya mbalimbali ya wilaya za Rorya na Tarime mkoani
Mara.
Amesema kuwa wamefanikiwa kuweka
alama mpya ndogo takriban 900 zenye umbile la pembe nne ambazo
zinaonana na kwamba sasa zinawezesha eneo la lote la mpaka wa kimataifa
mkoani Mara kuonekana kwa urahisi ambapo kazi hiyo imetumia muda wa
mwezi moja na majuma mawili.
Pamoja na kazi ya uwekaji wa
alama, pia kazi ya usafishaji wa eneo la mpaka kwa urefu wa mita tano
kwa kila upande wa nchi imefanyika kwa kufyeka miti na kuwezesha alama
hizo kuonekana kwa urahisi zaidi.
Bw. Marwa amesema kuwa hivi sasa
wameanza kazi mkoani Arusha baada ya kuruka kwa muda eneo la Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti mkoani Mara lenye urefu wa kilomita 51 kutokana na
mvua kuharibu barabara zinazotakiwa kufikisha vifaa vya ujenzi wa alama
pamoja na wataalam.
“Tumelazimika kuendelea na kazi
hii katika kijiji cha Ololosokwan kilichopo katika wilaya ya Ngorongoro
mkoani Arusha ambacho kimepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kisha
tutarejea nyuma kumalizia kipande tulichokiruka baada ya njia
zinazotusaidia kufikisha vifaa na wataalam hifadhini kuimarika.” Alisema
Bw. Marwa
Alisema kuwa tayari kilomita 21
zimefanyiwa kazi mkoani Arusha kwa hatua za awali kwa kuwa kazi hii
hufanyika kwa mpangilio wa timu zilizoundwa kitaalam hadi kufikia
uwekaji wa alama za mpaka.
Kazi ya uimarishaji wa mpaka kati
ya Tanzania na Kenya inayolenga kuwezesha Serikali kusimamia kwa
ufanisi shughuli za mipakani, rasilimali za nchi pamoja na ulinzi na
usalama ilianza katikati ya Mwezi Machi mwaka huu ambapo Kilomita 238
zinaimarishwa kutoka kando ya Ziwa Victoria mkoani Mara hadi Ziwa Natron
mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment