Watanzania hawajachoka kuishi kwa amani, lakini...
KATIKA
dunia hii kila jambo hutanguliwa na ishara. Nimepata kuandika, kuwa
Afrika mvua hainyeshi ghafla, utaziona ishara za mawingu.
Na nchi
nayo ni hivyo hivyo, ishara za nchi inayoelekea kubaya huonekana mapema.
Wahenga walituambia, kuwa ukiona zinduna na ambali iko nyuma.
Naingiwa
na shaka juu ya kuongezeka kwenye jamii, kwa kauli zenye kuashiria shari
zaidi kuliko maridhiano.
Na wananchi hawako katikati ya hili, bali
baadhi ya wanasiasa na wakati mwingine viongozi wa dini.
Ukweli
Watanzania walio wengi hawajachoka kuishi kwa amani, bali, kuna baadhi
ya wanasiasa na hata viongozi wa dini, kwa kutanguliza maslahi yao,
wanahangaika kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwa Watanzania. Kwamba
Watanzania wabaguane kwa misingi ya udini, siasa na hata ukabila.
Juzi
nimeandika makala kuzungumzia hatari ninayoiona katika hili la vyama vya
siasa kuanzisha vikosi ama vikundi vya ulinzi. Na ukweli ni kuwa, huko
nyuma niliandika juu ya hatari hii katika makala zaidi ya mbili za
magazetini, ni kuanzia mwaka 2001 pale CUF na CCM Zanzibar walipokuwa
kwenye msuguano mkubwa. Nikaandika tena baada ya Uchaguzi Mdogo wa
Arumeru Mashariki pale CCM na CHADEMA walipokwaruzana.
Na hapa
nitarejea moja ya mazungumzo muhimu ya kihistoria kupata bahati ya
kuyafanya; ilikuwa ni jioni ya Januari 24, 2012 pale nilipokutana na
Mama Mosi Tambwe ( sasa marehemu) nyumbani kwake Tabora Mjini.
Mosi
Tambwe aliingia TANU akiwa na miaka 18. Ni mmoja wa wanawake mahiri sana
kisiasa wa enzi hizo. Mosi Tambwe alinisimulia, kuwa alianzia kwenye
TANU Bantu Group, hiki kilikuwa ni kikundi cha vijana ndani ya TANU,
ambacho baadaye kikawa TANU Youth League.
Kwa
kirefu kabisa Mosi Tambwe aliniambia majukumu yao kama vijana kwa wakati
huo. Ni wakati nchi ikiwa chini ya mkoloni. Akanielezea pia majukumu
hayo yalivyobadilika baada ya uhuru. Enzi hizo vijana walikuwa
wakiandaliwa kupitia TANU Youth League ili waje kuwa makada wa chama,
hivyo basi, viongozi wa wananchi walinolewa vema. Walijengewa uwezo wa
kujenga hoja.
Ni enzi
hizo, baada ya kutoka Chipukizi, hatua iliyofuata ni Tanu Youth League.
Wengine wakaenda JKT na hata Jeshini. Azma kubwa ilikuwa kujenga
Uzalendo na Umoja wa Kitaifa.
Tumekosea wapi?
Jibu; ni
pale, kwa shinikizo la mabadiliko ya dunia , na kwa shingo upande, chama
tawala kiliporidhia kurejesha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. CCM
ikasahau kuratibu mabadiliko makubwa ya kikatiba ambayo yalipaswa
yaendane na mabadiliko hayo ya kimfumo.
Kimsingi,
hali tuliyo nayo sasa ya kuchanganyikiwa, hata kwenye hili la vyama
kuunda vikosi au la, inatokana na makosa makubwa, kama Taifa,
tuliyoyafanya mwaka 1992. Maana, ' Green Guards' katika mfumo wa chama
kimoja huenda haikuwa tatizo kubwa.
Nimeandika
mara kadhaa, kuwa historia ni mwalimu mzuri, lakini, wakati ni mwalimu
mzuri pia. Tujifunze kutokana na mabadiliko ya wakati. Katika wakati
tulio nao sasa, vyama vya siasa havipaswi kujiundia vikundi vya ulinzi
vyenye kupata hata mafunzo ya kijeshi. Ni ujasiri, kama viongozi wa sasa
watazipa mgongo fikra hizi za kizamani na kuendana na mabadiliko ya
wakati.
Tufanye nini?
Kama
ningeombwa ushauri hii leo, basi, ningevishauri vyama vya siasa, kuwa
kwa haraka sana, viachane na harakati za kuunda vikosi au vikundi vya
ulinzi. Jukumu hilo liachiwe vyombo vya usalama, hususan Jeshi la
Polisi, na hata makampuni ya ulinzi yenye kutambulika kisheria.
Na vile
vilivyopo vivunjwe. Maana, vikundi hivi vya ulinzi ambavyo kimsingi ni
vikundi vya wanamgambo wa vyama ni maafa tunayoyaandaa wenyewe. Kama
hatutanguliza busara na hekima, basi, itakuwa ni suala la wakati tu
kabla hatujajikuta kwenye dimbwi la maafa makubwa.
Tumeshaziona ishara.
Majuzi
nilikuwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kufuatilia kongamano la Amani ya
Nchi yetu kwa miaka 50 ijayo. Kwa masikitiko makubwa, ukumbi ule wa
Nkrumah haukujaa vijana.
Kwa vyama
vya siasa, badala ya kutumia muda na rasilimali zao kufyeka mapori ya
kuwaweka vijana kwenye ' makambi ya ukakamavu', umefika wakati sasa wa
kubadilika, kuachana na fikra hizo za kijima zenye kuturudisha nyuma
miaka 50.
Huu ni
wakati wa kuwajengea vijana wa vyama ' ukakamavu wa akili'. Na mahali
kama pale Nkrumah Hall ndipo vijana wa vyama walipaswa wahamasishwe
waende wakanoe akili zao. Waende wakajifunze kujenga na kubomoa hoja za
wengine kwa nguvu za hoja na si hoja za nguvu.
Zimepita, zama za ' Umkhoto we Sizwe'. Hizi ni zama za ' Umkhoto we Mitwe'- Ni mapambano ya kutumia vichwa kwa maana ya akili.
Naam, ukiona zinduna na ambali iko nyuma.
No comments:
Post a Comment