Pages

KAPIPI TV

Monday, June 18, 2012

WANAFUNZI WALEMAVU MAFINGA


Baadhi ya watoto wanafunzi mchanganyiko na wale wenye ulemavu wakiandamana katika maadhimisho hayo.
Na sisi tunahaki sawa kama walivyo wanafunzi na watoto wengine!
Siku ya Mtoto wa Afrika Oyeeeeeee!Nyuma ya wanafunzi hawa ni gari la kisasa limelotolewa kama msaada kwa Shule ya Msingi Makalala inayosomesha watoto wenye ulemavu.
Walemavu tukiwezeshwa tunaweza! Pichani aliyeshika kipaza sauti ni mmoja wa wanasheria wa CCBRT ambaye ni mlemavu wa macho.
Wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wakipewa tafsiri ya maneno kwa ishara katika maadhimisho hayo.

Na Joachim Mushi, Thehabari.com- Mafinga
Wanafunzi wenye ulemavu anuai katika Shule ya Msingi Makalala wameiomba Serikali na wadau wengine kuwasaidia kuwajengea mazingira bora ya kujifunzia kwa watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu bora kama ilivyo kwa watoto wengine.

Kauli hiyo imetolewa katika risala ya wanafunzi hao iliyosomwa Wilayani Mafinga kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika kiwilaya kwenye Shule ya Msingi Makalala nje kidogo ya Mjini wa Mafinga.

Katika maelezo yao watoto hao wameiomba Serikali na wadau wengine kuwatizama kundi la watoto wenye ulemavu anuai kwa jicho la karibu, hasa katika uboreshaji wa mazingira jumuishi ya kujifunzia katika shule zenye watoto wenye ulemavu.

Pamoja na hayo wanafunzi hao walemavu wameomba kuboreshewa mazingira ya lijifunzia katika Shule yao ya Makalala, ikiwa ni pamoja na kuwajengea chumba maalumu kwa ajili ya kujifunzia kitakachokidhi mahitaji ya kundi hilo maalumu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mafinga, Bi. Farida Mwasumilwe alisema licha ya Serikali kujitahidi kuboresha huduma mbalimbali kwa watu wenye ulemavu bado kuna changamoto nyingi hivyo kuomba wadau kushirikiana kwa pamoja kuwasaidia watu wenye ulemavu hasa watoto.

Bi. Mwasumilwe aliwataka wadau mbalimbali kusaidiana kutoa elimu kwa baadhi ya wazazi ambao bado wamekuwa na kasumba ya kuwaficha watoto wenye ulemavu ndani hivyo kukosa haki za msingi ikiwemo elimu, ambayo ndio mkombozi pekee kwa kundi hilo.

“Naomba tusaidiane kuwafichua watoto wote walemavu ambao baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaficha ndani hivyo kukosa haki yao ya msingi. Pia jamii haina budi kusaidia malezi ya watoto kwani mzigo huu sio waserikali pekee,” alisema Mwasumilwe ambaye ni Ofisa wa Elimu Shule za Msingi Wilaya ya Mafinga.

Katika maadhimisho hayo yalioambatana na michezo mbalimbali kwa makundi ya watu wenye ulemavu, Shirika la Sightsavers limeahidi kumalizia ujenzi darasa la kisasa pamoja na baadhi ya vifaa vya kujifunzia litakalokuwa na uwezo wa kufundishia wanafunzi wenye ulemavu shuleni hapo.

Shirika hilo mbali na kukabidhi fimbo 35 maalumu za kutembelea kwa wanafunzi wasioona pia limeahidi kutoa gari la kisasa kwa shule ya Makalala ili kuwasaidia wanafunzi walemavu hasa wasioona kupata huduma zao nje ya kituo hicho pale inapohitajika. (kila fimbo moja ina thamani ya sh 50,000 za kitanzania).

Maadhimisho hayo yaliandaliwa na taasisi anuai zinazofanya kazi na watu wenye ulemavu, zikiwemo Chama cha wasioona Tanzania (TLB), Kituo cha Habari Kuhusu Walemavu nchini (ICD), Sightsavers, CCBRT, INUKA, SHIVYAWATA kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu inasema, “Haki za Watoto wenye Ulemavu; Ni Jukumu letu Kuzilinda, Kuziheshimu, Kuziendeleza na Kuzitimiza”. 
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Kituo cha Habari Kuhusu Walemavu Tanzania (ICD)

No comments: