Pages

KAPIPI TV

Friday, June 29, 2012

WANAFUNZI VIJIJI VYA MILENIA MBOLA WAANZA KUTUMIA KOMPYUTA

 Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbola, Mrisho Rashidi(12) darasa la nne akiwa anafuatilia masomo yake kupitia kompyuta.
 Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Mbola,Bw.Hashim Ramadhani akiwa anamuelekeza  jambo mwanafunzi Mrisho Rashidi
 Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbola wakiwa wameketi nje ya majengo ya Shule yao.


Na Juma Kapipi-Uyui Tabora

Kwa kadri namna Utandawazi unavyozidi kuutawala Ulimwengu ndivyo mahitaji ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano yanavyozidi kuwa makubwa ukilinganisha na miaka michache iliyopita hapo nyuma.

Nadhani utakubaliana nami ninapoweka wazi kuwa matumizi ya kompyuta yalikuwa kwa sehemu kubwa ni katika maofisi zaidi kuliko maeneo mengine kama sijakosea sana.

Lakini hivi leo sasa imeanza kuwa kama vile ni maajabu  kwa Shule za Msingi na tena zilizopo vijijini,wanafunzi kuanza kutumia kompyuta kama nyenzo  muhimu cha kujifunzia.

Katika Shule za Msingi zilizopo eneo la Mradi wa vijiji vya Milenia Mbola tayari wanafunzi wameanza kujifunza na hatimaye kutumia kompyuta hali ambayo ukilinganisha na Shule za msingi zilizopo mjini Tabora ni tofauti kubwa kwakuwa si kitu cha ajabu kukuta mwanafunzi au mwalimu wa shule za msingi  mjini Tabora hajawahi hata kuigusa kompyuta.

Hali hii inanifanya nianze kuamini kuwa katika kipindi kifupi kijacho huenda  elimu na ujuzi wa mambo mbalimbali kwa wanafunzi wa vijijini hasa vijiji vya Milenia Mbola itakuwa ni moto wa kuotea mbali.

Likiwa bado nalifikiria hili lakini pia nakumbuka tukio jingine la wanafunzi wa shule hizi za vijiji vya Milenia Mbola la kuwasiliana kwa kupitia Spyper na wanafunzi wengine walioko Marekani katika Programu yao ya Connect to Learn ambayo pia wanaitumia kubadilishana uzoezi na wanafunzi hao wa Marekani jambo ambalo naliona kuwa ni jipya sana na pengine nalazimika kusema kuwa ni hatua ya Maendeleo.

Hivi ni kweli kwamba maendeleo ya aina hii yanaweza yakapatikana kwa maeneo yote ya mkoa wa Tabora au Tanzania kwa ujumla wake?na ni vipi yatafikiwa au ni kama ndoto tu eneo hilo moja la Vijiji vya Milenia Mbola?

Hapana fikra zangu kwasasa zinanielekeza kuwa kuna haja ya kujifunza haya mafanikio yanayopatikana katika vijiji hivi vya Milenia Mbola na si kukaa na kubweteka kuwa eti kwasababu kuna wafadhili wanasaidia kwa maana moja ama nyingine.

Licha ya kuwa kweli wapo wafadhili lakini cha msingi ni kuangalia fursa tulizonazo,na namna gani tutaweza kubadilisha changamoto kuwa mafanikio.

Kama ni wafadhili basi wamekuja kutuonesha njia nasi kuna haja ya kuifuata ili walau tuondokane na huu umasikini uliokithiri ambao tumekuwa tukiukumbatia pasipo sababu kiasi cha kushindwa hata kuwasaidia watoto wetu kupata elimu inayokwenda sambamba na huu utandawazi kama Teknolojia ya habari na Mawasilano Teknohama.

Jamani nina mengi ya kusema lakini acha niishie hapa neno langu ni moja tu,tuuangalie MRADI WA VIJIJI VYA MILENIA MBOLA kama darasa letu la kudumu kama kweli tunayodhamira ya dhati katika kuleta mabadiliko ya elimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

  


No comments: