Pages

KAPIPI TV

Saturday, May 26, 2012

CHAMA CHA KUTETEA HAKI ZA WANAUME WANAONYANYASWA NA WAKE ZAO TANZANIA CHAKUTANA SHINYANGA

 Baadhi ya wanachama wa Chama cha Kutetea Haki za Wanaume wanaonyanyaswa na Wake zao Tanzania walipokutana katika kikao cha dharura katika Hotel ya Karena mjini Shinyanga.
 Katibu wa Chama cha kutetea Haki za wanaume wanaonyanyaswa na wake zao Bw.Antony Sollo akizungumza katika kikao cha wanachama wa Chama hicho.
 Mwenyekiti wa Chama cha kutetea haki za wanaume wanonyanyaswa na wake zao Tanzania Bw.Belensi Alkadi akizungumza katika mkutano huo.
 Wanachama wa chama hicho wakijadiliana jambo.
 Wanachama wa Chama hicho wakisikiliza kwa makini


Na Mwandishi wetu Shinyanga.
Wanachama wa Chama cha kutetea haki za wanaume wanaonyanyaswa na wake zao Tanzania wamekutana katika kikao cha dharura mjini Shinyanga kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na mchakato wa kuandaa rasimu ya katiba na usajili wa Chama hicho chenye lengo la kuwatetea wanaume nchini wanaokabiliwa na manyanyaso dhidi ya wake zao.

Kikao hicho ambacho kimefanyika katika Hoteli ya Karena mjini humo,Katibu wa chama hicho Bw.Antony Sollo amesema Chama hicho kinatarajiwa kusajiliwa na kuzinduliwa rasmi mapema Julai mwaka huu hapa nchini na kwamba tayari hadi hivi sasa wanaume waliowengi wamekipokea na kuonesha dhamira ya kujiunga.

Amesema kuunda kwa Chama hicho kumetokana na ukweli kwamba idadi kubwa ya wanaume nchini wamekuwa wakinyanyaswa na hawana mahali pa msaada kwao hatua ambayo imekuwa ikiendelea kuwafanya kuwa wanyonge katika kukabiliana na matatizo ya manyanyaso waliyonayo.

Katibu huyo Bw.Sollo amefafanua kuwa vitendo vya manyanyaso kwa wanaume hapa nchini pia vimekuwa vikisababisha mauaji ya mara kwa mara na hata kuleta mfarakano ndani ya familia.

Amesema kuanzishwa kwa chama hicho pia kutasaidia kuimarisha mahusiano baina ya wanandoa kwakuwa wataishi kwa usawa huku wakizingatia haki na wajibu wa kila mmoja wao katika maisha ya kila siku.

Kwaupande mwingine mwenyekiti wa chama hicho Bw.Belensi amewataka wanaume nchini kukiunga mkono chama hicho ambacho kitakuwa ni kimbilio la wanaume na pia msaada kwa ngazi ya familia kutokana na migogoro inayojitokeza ndani ya ndoa.   


Miungoni mwa Masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kero ya wanaume kudharauliwa, kupigwa na wake zao kila siku na baya zaidi ni pale wanaponyimwa haki ya ndoa.

Mengine ni yanayohusu wanawake kubadili na kumiliki  haki na mali walizochuma pamoja na wenzi wao hatua ambayo pia imeonekana kikwazo kwa wanaume.

Huu ulikuwa ni mkutano wa pili tangu kuanzishwa kwa mchakato  wa chama hicho jijini Dar-es-salaam.

 

No comments: