Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevill Meena (kushoto)
akijadiliana jambo na Mratibu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa
TGNP, Bi. Lilian Liundi. Kulia ni mmoja wa maofisa wa TGNP kutoka
kitengo cha Habari.
Picha ya pamoja kati ya wahariri mbalimbali walioshiriki katika semina
hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya (wa kwanza kulia
aliyechuchumaa)
Na Mwandishi Wetu
MTANDO wa Jinsia
Tanzania (TGNP) umetoa maoni ya jumla ambayo wangependa yaingizwe kwenye
mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya ya Tanzania. Maoni hayo yalitolewa na TGNP
kwenye semina ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Akizungumza jana
jijini Dar es Salaam katika semina hiyo, Mratibu wa Kitengo cha Habari na
Mawasiliano wa TGNP, Bi. Lilian Liundi alisema madaraka katika muhimili wa
utawala wa sasa ni makubwa hivyo kushauri yapunguzwe na kuwe na utengano kati
ya mihimili mikuu mitatu ya nchi.
Bi. Liundi pia
ametaka uwepo wa uwiano sawa wa kijinsia (50/50) huku akitaka mawaziri wasiwe
wabunge na uwepo wa utaratibu wa viongozi (wabunge, madiwani) kuwajibishwa
katikati ya mihula tofauti na ilivyo sasa.
Aidha mambo
mengine ambayo Bi. Liundi ameyatoa kama changamoto na kushauri yaingizwe kwenye
mchakato wa Katiba Mpya ni pamoja na kufutwa kwa adhabu, uwepo wa uhuru wa
kupinga matokeo ya urais baada ya kutangazwa na ukomo wa uongozi wa wabunge, madiwani na serikali za mitaa.
Amesema siasa za
uliberali mamboleo zilizoletwa na
mataifa ya nje katika nchi za
kiafrika zimesababisha mtafaruku mkubwa katika siasa za kiafrika, hali ambayo imezua
migomo na mapambano dhidi ya uporaji wa rasilimali, ubinafsishaji wa huduma za
afya na kuzifanya kama bidhaa na uporaji mkubwa wa ardhi na madini.
“Harakati hizi
zimesababisha makundi ya kijamii, vyama vya siasa na wanaharakati kuanza kudai
mabadiliko ya katiba katika nchi zao. Mfano mzuri ni nchini Kenya 2007,”
alisema.
Pamoja na hayo
alisema licha ya mchango mkubwa unaotolewa na wanawake nchini Tanzania bado
hakuna fursa sawa kimgawanyo wa masuala mbalimbali.
Asilimia 80 ya nguvu kazi vijijini ni wanawake
na asilimia 60 yao ni wazalishaji wa chakula. Wanawake ambao hawana ajira ni asilimia
40.3 (2006) ukilinganisha na wanaume ambao walikuwa asilimia 19.2 ( 2006),
asilimia 66 ya wanawake wanafanya kazi zisizokuwa na kipato (kazi za huduma)...
asilimia 39.5 ya wanawake hawajasoma ukilinganisha na asilimia 25.3 ya wanaume...,”
Awali akitoa mada
katika semina hiyo ya wahariri, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema
licha ya uwepo wa maendeleo kwa kiasi fulani ukilinganisha na miaka ya nyuma,
bado kuna mifumo kandamizi inayoikabili jamii ya kipato cha chini.
Alisema maendeleo
ya huduma za jamii katika maeneo mbalimbali kwa kiasi kikubwa yanawanufaisha
zaidi wenye nacho (matajiri) na si masikini. “Huduma za jamii zimeongezeka
ndiyo lakini wanaonufaika zaidi na huduma hizo ni wachache...ukiangalia utaona
Serikali inawajibika zaidi kwa wafadhili na si wananchi wake...,” alisema Bi. Mallya.
Alioneza kwa sasa
hata tabaka la wasionacho na walionacho ni kubwa ukilinganisha na miaka ya
nyuma huku jukumu la kuihudumia jamii likirudi kwa familia zenyewe (majumbani)
na si Serikali walioiweka madarakani kuwahudumia wananchi wake.
No comments:
Post a Comment