KAMATI YA MAZISHI YA MSANII STEVEN CHARLES KANUMBA
Taarifa kwa vyombo vya habari
APRILI 9, 2012
Msanii wa filamu, aliyebeba mapenzi
makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa jumla, Steven Charles
Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012, atazikwa kesho
Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mazishi ya Kanumba, yamepangwa na
kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu, mapenzi yake kwa watu na
hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya wengi kumuaga
msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda wote wa
Afrika Mashariki na Kati.
Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa
kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo
katika tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye
maisha ya milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye
shughuli nzima.
RATIBA
Mwili wa marehemu Steven Kanumba
utachukuliwa kwa msafara kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30
asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi
hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea
itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga.
Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa
wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi, wakijipanga kando ya Barabara za Umoja
wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima mwili wa Kanumba
wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.
Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba
utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi
wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib
Bilal.
Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa
ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka
kwa watu mbalimbali.
Saa 6:00 mchana, ratiba ya kumuaga
Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati
wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya
Kinondoni, msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya
Kinondoni kuelekea makaburini.
Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya marehemu.
Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu
watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili
kumuaga kwa heshima.
Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote
tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee kuwa nasi siku zote ila
Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Jina lake
lihimidiwe.
K.N.Y GABRIEL MTITU
MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI
No comments:
Post a Comment