Pages

KAPIPI TV

Friday, April 27, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI SHUTUMA DHIDI YA WAZIRI WA FEDHA KUHUSIKA KUUZA KIWANJA BILA UTARATIBU CHA CHC NAMBA 10



UTANGULIZI
1.0             Wakati PSRC ilipokuwa chini ya Wizara ya Mipango na Ubinafsishaji, mwaka 2002 iliuza kiwanja Na. 192 kwa Mohamed Enterprise (T) Limited (METL) na mwaka 2003 ikauza kiwanja Na. 191 kwa Dar es Salaam RTC. Viwanja hivyo viliuzwa kabla ya PSRC kuvunjwa tarehe 31 Desemba, 2007 na shughuli zake kukabidhiwa CHC tarehe 1 Januari, 2008, ambapo ndiyo shughuli za CHC zilihamishiwa Wizara ya Fedha. 

Kiwanja Na. 192 (au Na. 11 kwa sasa), cha GAPEX (iliyovunjwa na baadhi ya mali zake kukabidhiwa PSRC) na kiwanja Na. 191 cha Dar es Salaam RTC, vilikuwa katika eneo moja vikitumia barabara moja kuingia kwa kupitia ndani ya kiwanja Na. 191 kutokea barabara ya Nyerere (Pugu Road).  Hata hivyo, PSRC waliuza viwanja hivyo bila kwanza kutoa njia (access road) kuingia kiwanja Na. 192.

2.0             Dar es salaam RTC walianza kupatiwa hati ya kiwanja Na. 191, hivyo kukawa na mgogoro wa muda mrefu kwa sababu METL hakuweza kupatiwa hati na Manispaa ya Temeke bila ya kuwa na njia. Vile vile Dar es Salaam RTC kutokana na kero ya magari makubwa ya METL, walikataa yasiendelee kupita katika kiwanja chao bila malipo. Malipo ya madai ya Sh. 2.34bn ya barabara yanayodaiwa na Dar es Salaam RTC hayakuwahi kulipwa na Serikali hadi sasa.

3.0             Kwa misingi hiyo PSRC ilitakiwa kutoa access road kwa METL. Kamati ya Serikali chini ya CHC ilitafakari suala hilo nakuona kwamba, kiwanja Na. 10 ambacho kiliwekwa chini ya PSRC kupitia mali za TANGOLD iliyokuwa kampuni tanzu ya NMC, kingeweza kutumiwa kutatua tatizo hilo. Kiwanja Na. 10 kilikuwa kimepangishwa kwa M/s Noble Azania Investment Ltd (NAIL) na aliweka pingamizi asinyang’anywe na PSRC.  METL alikubali kwamba endapo atapewa kiwanja hicho ili apate barabara atachukua na kesi na madai ya NAIL.

4.0             Katika Mkutano wake wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, masuala kadhaa yalijitokeza na kujadiliwa.  Aidha, katika majadiliano hayo baadhi ya waheshimiwa wabunge walichangia hoja za POAC na PAC kwa kumshutumu Mhe Waziri wa Fedha. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakichangia hoja walisema kuwa, baadhi ya Mawaziri ni wezi na kuwa wanatafuna fedha za Watanzania bila ya woga, na kuwa Mhe. Waziri wa Fedha ameuza viwanja vya CHC. Aidha, walidai kuwa, alihusika katika uuzaji wa mali ya Serikali katika kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere na kwamba ameingilia utendaji wa Mashirika ya Serikali ikiwamo CHC. 

5.0             Tungependa kutoa ufafanuzi kuhusu hoja hizo kama ifuatavyo:- Kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere hakikuuzwa na Wizara ya Fedha, wala na Waziri wa Fedha. Kiwanja hicho kiliuzwa na aliyekuwa Mwenyekiti na Kaimu Mkurugenzi wa CHC kinyume na maelekezo ya Wizara ya Fedha na Kamati ya Wataalam (DTT), kwamba kiwanja hicho kiuzwe kwa bei ya soko kwa kuzingatia Sheria na Taratibu.

6.0             Ukweli upo kwamba, baada ya maelekezo ya Wizara ya Fedha kwamba bei ya soko na taratibu na sheria zitumike, Kamati ya Wataalamu wa Serikali, ilikaa na kushauri kwamba taratibu na sheria ni kutangaza ili kupata bei ya soko.

7.0             Bodi ya CHC ilikaa na kujadili maelekezo ya Wizara ya Fedha na ushauri wa Kamati ya Wataalam. Baadhi ya Wajumbe wa Bodi walishindwa kuelewa maana ya taratibu na sheria na bei ya soko, hivyo Bodi iliagiza Waziri wa Fedha aombwe ufafanuzi. Mwenyekiti na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC walitumwa na Bodi wamwone Waziri wa Fedha ili warudishe majibu kwenye Bodi. Waziri wa Fedha alitoa maelezo kwao kwamba, tayari alishatoa maelekezo kwa maandishi hivyo waendelee kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.

8.0             Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC hawakurudi kwenye Bodi baada ya kupata ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Fedha, bali waliamua kuuza kiwanja hicho kwa bei ya Mtathmini, badala ya kutangaza na kupata bei ya soko kama walivyoelekezwa na Wizara ya Fedha na Kamati ya Wataalam. Aidha, hawakurudi kwa Wizara ya Fedha kutoa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Wizara.

9.0             Aidha ni vyema ijulikane kwamba, ukaguzi maalumu uliofanywa huko CHC na Mkaguzi wa Nje, wakati wote wa ukaguzi Wizara ya Fedha haikuhusishwa kutoa ufafanuzi au taarifa yoyote.       

10.0         Tuhuma kuhusu kwamba, Wizara ya Fedha ilihusika katika uuzwaji wa kiwanja hicho kwa kutoa maagizo kwa uongozi wa Shirika kuuza kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere bila kuishirikisha Bodi ya Wakurugenzi, hazina ukweli.
11.0         Hakuna maagizo yoyote ya Wizara ya Fedha yanayosema kuwa, kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere kiuzwe kwa kampuni ya METL kwa kiasi cha shilingi bilioni 2.46 bila kuzingatia sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2006.

12.0         Kwa kuzingatia maelekezo ya Waziri wa Fedha ni dhahiri kuwa, Mhe. Waziri wa Fedha, hakuhusika na uuzaji wa kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere na wala hakuingilia utendaji wa CHC. Maelekezo aliyotoa yaliitaka CHC ifanye maamuzi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni.

Badala yake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC waliamua kuuza kiwanja hicho bila kuzingatia ushauri wa Kamati ya Wataalam (DTT) na maelekezo ya Wizara ya Fedha.

13.0         Kwa misingi hiyo, tuhuma kwamba, Mhe. Waziri wa Fedha alihusika na uuzaji wa kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere sio za ukweli.


KATIBU MKUU
WIZARA YA FEDHA
APRILI, 2012

No comments: