Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa
Shirikisho la Filamu Tanzania –TAFF- kuomboleza kifo cha msanii maarufu
nchini Steven Charles Kanumba, aliyeaga dunia usiku wa kuamkia leo,
Jumamosi, Aprili 7, 2012.
Katika
salamu hizo, Rais Kikwete amemwomba kiongozi huyo wa TAFF kufikisha
salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wana-familia ya Kanumba
na kwa wasaani wote nchini ambao wamepotelewa na mdau na mwenzi wao.
Rais
Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuzunishwa na kifo cha msanii huyo
ambaye amemwelezea kuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye
katika uhai wa maisha yake mafupi na akiwa bado kijana sana amechangia
kwa kiwango kikubwa maendeleo ya sanaa ya filamu nchini na kupitia sanaa
hiyo kuitangaza Tanzania kimataifa.
Amesema Rais: ”Nimepokea kwa mshtuko na
huzuni nyingi taarifa za kifo cha Ndugu Steven Charles Kanumba. Kupitia
filamu zake, ameburudisha na kuelimisha jamii yetu kwa namna ambayo
haiwezi kupimika. Alikuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye
mchango wake mkubwa katika kuanzisha, kukuza na kuimarisha sanaa ya
filamu nchini hautasahaulika.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Ndugu
Kanumba pia ametoa mchango mkubwa katika kuitangaza nchi yetu ya
Tanzania mbele ya mataifa mengine kupitia sanaa ya filamu na uwezo
mkubwa wa kisanii. Tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake huo kwa nchi
yetu.”
“Nakutumia
wewe Rais wa TAFF salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa
wasanii wote wa filamu na sanaa nyingine kufuatia msiba huu mkubwa kwa
fani yetu ya sanaa. Aidha, naomba unifikishie salamu za dhati ya moyo
wangu kwa wanafamilia wote. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu
mkubwa. Waambie naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha msiba,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Namwomba Mwenyezi Mungu awape subira na
nguvu za kuweza kuhimili kipindi hiki kigumu kwa sababu yote mapenzi
yake. Aidha, naungana na wana-familia na wasanii wote nchini kuwomba
Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu
Steven Charles Kanumba. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
07 Aprili, 2012
No comments:
Post a Comment