Koplo Othman Daima wa Kikosi
cha Usalama Barabara Zanzibar akitoa elimu ya matumizi salama ya
barabara kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kiembesamaki mjini Zanzibar.
|
Sajent Ali Khasim wa Kikosi cha Usalama Barabarani Zanzibar akitoa elimu juu ya matumizi Salama ya Barabara kwa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kiembesamaki mjini Zanzibar. |
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
Jeshi la Polisi Zanzibar limesema kuwa
limekuwa likiwatumia Askari Polisi waliopangwa kufanya kazi kwa wananchi
kama Polisi Shehia katika mpango wa uvushaji wa wanafunzi barabarani
wanapokwenda na kutoka shuleni ili kuwaepusha na ajali za barabarani.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed,
amesema kuwa, Askari Polisi hao pia wamekuwa wakitoa msaada kama huo kwa
vikongwe wasio na uwezo wa kuvuka wenyewe barabara.
Amesema
kabla ya kuanzishwa kwa utaratibu huo, kumekuwapo na matukio mengi ya
ajali za barabarani ambazo nyingi zilikuwa zikisababisha vifo na vilema
vya kudumu kwa watumiaji wa barabara wakiwemo wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari.
Kamanda
Aziz amesema sambamba na mpango huo, lakini pia Askari Polisi wa
Usalama Barabarani wameendelea na mpango wake wa kutoa elimu ya matumizi
salama ya barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa usalama kwanza ili kupunguza ajali.
Amesema
kwa kufahamu kuwa wanafunzi wa leo ndio wazazi na walezi wa kesho,
Jeshi la Polisi mkoani huo limeamua kutilia mkazi katika kutoa elimu kwa
wanafunzi hao ili kuwajengea uwezo wa kuzifahamu sheria mbalimbali
zikiwemo za matumizi salama ya barabara.
Kamanda
Aziz amesema kuwa mpango wa utoaji wa elimu kwa wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari unafanywa na askari wa Kikosi cha Usalama barabarani
wakiwemo maafisa wa kikosi hicho kama sehemu ya uwajibikaji.
Amesema
mara nyingi Askari hao wamekuwa wakienda katika shule mbalimbali kutoa
elimu hiyo ili kuwawezesha wanafunzi sio kuelewa tu matumizi samala ya
barabara lakini pia madhara yatokanayo na ajali za barabarani.
Amesema
ajali za barabarani zimekuwa zikipoteza maisha ya watu wengi na wengine
kwa mamia wakibaki na vilema vya kudumu na wengine hata kushindwa
kufanya kazi za uzalishaji mali na kumudu jitunza wao wenyewe pamoja na
kuzitunza familia zao na hivyo kupunguza pato la taifa.
Kamanda
Aziz alikuwa akizungumza na mwandishi wa Habari hizi aliyetaka kujua
mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo katika mkoa
wa Mjini Magharibi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment