Pages

KAPIPI TV

Thursday, April 19, 2012

JINAMIZI LA MILLYA:DIWANI WA CCM MWANZA AJIUNGA NA CHADEMA


UPEPO mbaya unaonekana kukikumba Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa viongozi wake kukihama chama hicho, umeingia katika Mkoa wa Mwanza, ambapo Diwani wa Kata ya Nyampulukano Wilayani Sengerema mkoani hapa, Hamis Mwangao Tabasamu ametangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema.

Diwani huyo ambaye amejipambanua kwa kupiga vita ufisadi ndani ya wilaya hiyo, ametangaza azma yake hiyo katika kikao na waandishi wa habari kilichofanyika Ryan's hoteli, na kupokelewa na aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema).

Diwani Tabasamu ambaye jumamosi amepanga kuhudhuria na kuhutubia mkutano mkubwa utakaoongozwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa kata ya Nyampulukano, amekuwa ni miongoni mwa viongozi wengine wa CCM kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema ndani ya muda wa wiki moja.

Hivi karibuni, aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mkoa wa Arusha, James Milya alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote kisha kujiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Mbali na Milya, viongozi wengine kadhaa akiwemo diwani wa Kata ya Sombetini mkoani Arusha, Alphonce Mawazo (CCM), juzi alikihama chama chake hicho kisha kujiunga na Chadema, chama ambacho kinaonekana kuiweka pabaya CCM na Serikali yake kwa ujumla.

Akizungumza mchana huu wa leo, katika kikao chake na waandishi mbele ya Lema ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa, diwani Tabasamu ambaye aliwahi kuibua tuhuma za ufisadi katika halmashauri ya Wilaya ya Sengerema alisema: "Kuanzia leo (jana), natangaza rasmi kukuhama CCM na kujiunga na Chadema".

Alisema, lengo lake la kuhama kutoka ndani ya CCM si la kushawishiwa na mtu ama kiongozi yeyote, bali ni dhamira yake ya kweli kama Mtanzania halisi mwenye uhuru wa mawazo, na kwamba amechoshwa na siasa za 'majitaka' ndani ya CCM.

No comments: