Mkuu wa mkoa wa Tabora Bi.Fatma Mwassa amezitaka halmashauri
za wilaya mkoani humo kuongeza juhudi katika kuihamasisha jamii kujiunga na
mfuko wa Afya ya jamii ikiwa ni hatua
muhimu ya kuwawezesha kupata huduma ya matibabu kupitia mfuko huo.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya uliofanyika mjini Tabora,mkuu huyo alisema halmashauri na wadau
wengine wa mfuko huo wanaowajibu katika
kuuelimisha umma kuhusu mfuko huo ikiwa ni hatua muhimu ya kufanikisha dhamira ya Serikali kwa kila mtanzania kuwa kwenye utaratibu wa
Bima ya Afya.
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa gharama za matibabu
zimekuwa zikipanda mara kwa mara huku akibainisha kuwa njia pekee ya kumkomboa
mtanzania ni kumpa uhakika wa kutibiwa yeye pamoja na familia yake kupitia
mfumo wa Mfuko wa Afya ya jamii ambao unaratibiwa na NHIF.
Pamoja na kuainisha masuala kadhaa ya faida za mFuko huo
Mkuu huyo wa mkoa alitoa mfano kwa nchi nyingi duniani zimekuwa zikifanikiwa
katika masuala ya Afya kupitia Mifuko ya aina hiyo.
“Kwa wenzetu suala la Bima ya Afya ni la lazima kwa kila
mtu,hata kwa wengine wanaopata fursa ya kwenda nje ya nchi kusoma ni lazima uwe
umejiunga vinginevyo hutaweza kupokelewa”alisema Bi.Fatma Mwassa
Hata hivyo kwa upande mwingine mkuu huyo alionesha
masikitiko yake juu ya uchangiaji mdogo wa huduma ya Mfuko wa Afya ya Jamii CHF huku akianisha takwimu zinazoanzia Januari
2012,ambapo kati ya kaya 410,148 zilizopo mkoani Tabora ni kaya 14,860 tu ndizo
zilizojiunga na mfuko huo ambayo ni sawa na asilimia 3.6.
Aidha pamoja na kuwa mkoa wa Tabora ndio chimbuko la la
Mfuko huo wa Afya ya Jamii CHF ambao ulianzia wilayani Igunga kwa halmashauri
zote hapa nchini lakini jambo la kushangaza bado halmashauri nyingine zilizopo
mkoani Tabora zinashindwa kufanya vizuri katika kufikia lengo lililowekwa na
Serikali.
Kwaupande mwingine mkuu huyo wa mkoa Bi.Fatma alilazimika
kuwataka wadau na halmashauri kwa ujumla kutumia vikundi vya ushirika pamoja na
vyama vya msingi kama njia muhimu itakayosaidia kuandikisha wananchi waliowengi
kujiunga na CHF.
Mkutano huo wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulihudhuria
na baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu kitaifa wa NHIF,Katibu tawala mkoa wa
Tabora,Wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Tabora,waheshimiwa wabunge,Viongozi wa
halmashauri za wilaya na manispaa wakiwemo madiwani na wadau wengine wa Afya
pamoja na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment