Ndugu zangu,
Katika
dunia hii mwanadamu huwezi kumchagua jirani yako. Jirani yako ni jirani
yako. Msiba wa jirani ni msiba wako pia, unakuhusu.
Maana,
kuna wanaohoji JK kuacha mambo ya nyumbani na kwenda kushiriki maziko
ya Bingu wa Mutharika. Silioni kosa katika hilo. Na hata kama JK
angeamua kutokwenda mazikoni Blantyre, bado, asingekwepa lawama. Maana,
kuna ambao wangemlaumu JK kwa kutozingatia mila na desturi zetu
Waafrika; kushiriki kwenye kumzika jirani yako.
Tukumbuke,
kuwa Wamalawi si tu ni jirani zetu, ni ndugu zetu pia. Kuna Wanyasa
wengi wa Malawi katika nchi hii waliochanganyika na makabila yetu. Na
tunaambiwa, kuwa siku ya mkesha wa Uhuru wa Malawi, Watanzania wengi
kando ya Ziwa Nyasa nao walikesha wakishangilia. Uhuru wa Mnyasa ni
Uhuru wetu. Msiba wa Mnyasa, ni msiba wetu.
Mengineyo…
Nchi
yetu inapita sasa kwenye kipindi kigumu sana. Tusishushe chini kiwango
cha mjadala. Kubaki kumjadili JK na safari kwenda kutuwakilisha mazikoni
ni kushusha kwa makusudi kiwango cha mjadala. Kwa makusudi tutakuwa
tumeacha kujadili hoja za msingi ikiwamo hii ya kashfa za ufisadi wa
kutupwa uliodhihiri bungeni na unaotutaka tuweke shinikizo kwa wahusika
kuachia ngazi na hata kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Maana,
anayeliibia taifa ni mhalifu tena zaidi ya mwizi wa kuku. Huyu ni
jambazi. Kumwacha aendelee kukalia ofisi ya umma ni sawa na kumsusia
mlevi bia, au kumpa fisi kazi ya kulinda bucha.
Tuliko
sasa ni kubaya. Tunakokwenda kutakuwa ni kubaya sana kama hatutachukua
hatua sasa. Nimeona asubuhi ya leo kwenye runinga ( Channel Ten)
utetezi wa ajabu kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi Bw. Omar Nundu.
Nundu
anadai hawezi kujiuzuru kwa kutoa hoja ambazo kimsingi zinamtaka aachie
ngazi haraka iwezekanavyo ili abaki na heshima kwa jamii kama bado
anayo.
Anatwambia
Watanzania kuwa amekuwa ‘akizungukwa’ na Naibu wake Athuman
Mfutakamba. Ndio, Waziri Nundu anapojitetea kwa Watanzania kwa kusema
haelewani na Naibu wake na kuwa kampuni ya Kichina ilimpeleka Naibu
wake China, Mauritania na Equatorial Guinea bila kibali chake inatosha
kuonyesha kiwango cha juu cha ukosefu wa nidhamu, uwajibikaji na
uadilifu katika baraza la mawaziri . Sioni ni kwa namna gani maelezo ya
Nundu yanaweza kumlinda mbali ya kuonyesha ulazima wa kuwajibishwa
kwake haraka iwezekanavyo.
Ndio
huwezi kuonyesha kuwa ulijua kilichokuwa kikifanyika, ukabaki kimya
mpaka unatwambia hii leo, halafu utake ridhaa ya umma ikuamini kuendelea
kukupa dhamana ya kushika nafasi hiyo hiyo.
Na wahenga walisema; kwenye msako wa nyani ngedere hawezi kusalimika.
Ndio,
tutafanya makosa kudhani kuwa ’madudu’ haya yaliyoibuliwa kwenye ripoti
ya CAG yanahusu Wizara tano au sita tu. Hii ni fursa pekee kwa
Watanzania kupitia wabunge wao kuendesha ’ msako mkubwa’ wa wote wenye
kulitafuna taifa letu tunalolipenda.
Ni
wakati pia wa kuhakikisha Katiba Mpya tunayokwenda kuitolea mapendekezo
yetu itusaidie kuziba mianya ya wezi wa mali ya umma kuendelea
kuliibia taifa bila ya hofu ya kufikishwa mahakamani na hata kutiwa
magerezani.
Ndio,
hatuwezi kuenenda kama tunavyoenenda sasa; maana, unapoona Wananchi
wanalalamika, Wabunge wanalalamika, Mawaziri wanalalamika, na Rais
analalamika, basi, hilo ni taifa la ajabu sana. Taifa la Walalamikaji.
Na
maradhi ya ‘ kulalamika’ ni ya kimfumo. Ni mfumo mbovu tu ndio
unaoweza kuzaa Taifa la Walalamikaji. Turekebishe mfumo wetu kwa kupitia
Katiba. Inawezekana.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
No comments:
Post a Comment