Mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone akizungumza kwenye kikao cha kamati ya bunge, katiba na utawala, kilichofanyika ofisini kwake. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa kamati ya bunge, katiba na utawala Angella Kariuki. (Picha na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu.
Mkuu wa mkoa wa SIngida Dk. Parseko Kone ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kubadilisha jina la Katibu tawala mkoa na kurejesha jina la mkurugenzi wa maendeleo wa mkoa (RDD) ili kurahisisha utendaji kazi wa sekretarieti mkoa.
Dk. Kone ametoa mapendekezo yake mbele ya kamati ya bunge ya katiba, sheria na utawala iliyokuwa kwenye ziara ya siku moja ya kikazi mkoani Singida.
Aidha amesema chini ya RDD, kuwe na wakuu wa idara zinazojitegemea lakini zikiwa zinawajibika moja kwa moja kwa mkurugenzi wa maendeleo mkoa.
Akifafanua zaidi, amesema kamati ya ushauri ya mkoa itapewa nguvu zaidi endapo itakuwa  kamati ya maendeleo ya mkoa, badala ilivyo sasa ambapo ni kamati ya ushauri tu.
“Kwa sasa mkuu wa mkoa ni mwenyekti wa kamati ya ushauri ya mkoa, hivyo anaingia moja kwa moja kwenye kundi la ushauri tu na si kusimamia” amesema.
Amesema kitendo cha mkuu wa mkoa kuwa mshauri tu, kinakinzana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 61(4).
Dk.Kone amesema ibara hiyo inaeleza kuwa mkuu wa mkoa atakuwa ana wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Dk. Kone amependekeza makatibu tawala mkoa, wakurugenzi wa wilaya, majiji na manispaa warejeshewe mamlaka ya nidhamu kwa watumishi walio chini yao.