Mkuu wa wilaya ya Tabora Bw.Moshi Chang'a amewaonya walimu wa shule za sekondari na vyuo kuacha tabia ya kuwahubiria mambo ya vyama vya siasa wanafunzi muda wa masomo kwakuwa wanatumia muda mwingi kuwakosesha taaluma kwa kuzungumzia masuala ya wanasiasa na vyama vyao.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kuweka jiwe la msingi ukumbi wa kufanyia mitihani wa Shule ya Sekondari ya New Era mjini Tabora,Bw.Chnag'a alikemea tabia hiyo iliyoanzishwa na baadhi ya walimu wanapoingia madarasani na kuonya kuwa mwalimu atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu pasipo kujali shule anayofundisha ni ya serikali au ya mtu binafsi.
Alisema walimu wamekuwa wakitumia muda wa masomo kuwaongelea mambo ya siasa wanafunzi na matokeo yake wanafunzi wanashindwa kufanya vizuri katika masomo na mitihani ya Taifa.
Aidha ingawa hakuzitaja shule au walimu ambao wamekuwa na tabia hiyo lakini akasisitiza kuwa serikali itawachukulia hatua walimu hao na kwamba hadi sasa tayari majina ya walimu hao yanafahamika.
Kwaupande mwingine mkuu huyo wa wilaya amewataka wanafunzi kujibidiisha katika masomo na kutojihusisha na masuala ambayo yatavuruga utaratibu wa masomo yao ikiwa ni pamoja na kuwa mbali na masuala ya migomo isiyo na faida kwao.
No comments:
Post a Comment