Na Allan Ntana, Tabora
KANISA
la Free Pentecost Church of Tanzania (FPCT) limekemea vikali watu wote
wanaojihusisha na vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya watu wenye
ulemavu wa ngozi (albino) ambavyo vinazidi kushamiri hapa nchini.
Hayo
yalijiri jana katika ibada maalumu ya uzinduzi wa kanisa hilo lililopo
katika mtaa wa Kilolelini katika Manispaa ya Tabora iliyoongozwa na
Askofu Wilson Lazaro ambaye ni Makamu Askofu Mkuu wa FPCT hapa nchini,
ibada hiyo iliambatana na tukio la kusimikwa Mchungaji Kiongozi wa
kanisa hilo Peter Shani na timu ya watendaji wa kanisa.
Akihubiri
katika ibada hiyo Askofu Lazaro alisema vitendo vya ukatili
wanavyofanyiwa wanadamu wenye ulemavu wa ngozi havipaswi kufumbiwa macho
kwani vinafanywa na watu wasiotaka kutembea na Mungu katika maisha yao
hivyo ni lazima tuvikatae na tuvikemee vikali makanisani na nje ya
kanisa.
‘Tunakataa
vitendo vyote vya ukatili na mauaji dhidi ya albino, katika jina la
YESU kristo, watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo popote walipo
washindwe…. tunawakemea kwa mamlaka ya jina la YESU kristo’, haya ni
maneno yaliyojiri katika maombi yaliyoongozwa na Askofu Lazaro.
Alisema
katika kizazi hiki wanadamu wengi wanampenda sana Mungu lakini tatizo
lililopo hawataki kutembea naye katika maisha yao yote na katika
shughuli zao za kila siku jambo ambalo linaongeza uadui, chuki na
uharibifu mkubwa.
Aidha
alifafanua kuwa thawabu, hekima na utajiri vinatoka kwa Mungu na sio
kwa wanadamu, japokuwa wanadamu wengine leo hii wanahangaika kutafuta
utajiri usiku na mchana kwa waganga wa kienyeji ambao huwaelekeza kwenda
kuleta viungo vya albino ili wapate utajiri, hii sio sawa.
‘Tukitaka
kufanikiwa ni lazima tutembee na Mungu katika maisha yetu, hata hili
kanisa lenu mkitaka baraka zimiminike na mzidi kufanikiwa zaidi ni
lazima mtembee na Mungu, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Waebrania
11:5-6’, alisema.
Akizungumzia
mchakato wa kupata katiba mpya unaoendelea hivi sasa hapa nchini Askofu
alitoa wito kwa kila Mkristo kumwomba Mungu ili atuwezeshe kupata
katiba bora itakayokidhi matakwa ya kila Mtanzania katika nyanja
mbalimbali za kiuchumi, kielimu, kisiasa na kijamii.
Awali
akisoma risala ya kanisa kwa mgeni rasmi (Askofu Lazaro), Mchungaji
Kiongozi wa kanisa la FPCT Parishi ya Tabora Mch.Elias Shijja alisema
kanisa la Kiloleni lenye waumini 494 sasa tangu lianzishwe mwaka 1983
limekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mapato ya kanisa
ambapo yalifikia kiasi cha sh 23,867,600 kwa mwaka.
Alitaja
mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kupata jengo la kuabudia ambalo
sasa liko mbioni kupanuliwa zaidi, kupata waalimu 26 wa shule ya
jumapili, wainjilisti 9, mashemasi 16, wazee wa kanisa 4 na kuongezeka
watoto wa shule ya jumapili hadi 138 sasa.
Naye
Askofu wa kanisa hilo jimbo la Tabora Jeremiah Mnangala alibainisha
kuwa kasi ya kukua kwa kanisa hilo katika mkoa huo inaridhisha sana
kwani awali walikuwa na parishi mbili tu za Yerusalemu na Ng'ambo na
jumla ya makanisa 11 lakini sasa wamepata parishi ya tatu ya Kilolelini
na idadi ya makanisa yao sasa imefikia 18.



No comments:
Post a Comment