Pages

KAPIPI TV

Saturday, July 21, 2012

NAENDESHA MAISHA NA FAMILIA YANGU KWA KUUZA KAHAWA"Osama"

Bw.Ramadhan Bashahu Nyamweru,mkazi wa manispaa ya Tabora akiwa katika kibanda chake cha kuuzia Kahawa eneo la Stendi ya zamani ya mabasi.

Na Hastin Liumba,Tabora

AJIRA ya mwenyezi Mungu,haiko katika elimu ya utawala.....bali ipo
katika kile alichoandaa Mungu ili kila mtu aishi maisha bora.

Hii ni kauli ya Ramadhan Bushahu Nyamweru,(55), maarufu kama
''Osama",mkazi wa manispaa ya Tabora,ambaye anafanya biashara ya kuuza
kahawa katika kibanda chake eneo la stendi ya mabasi zamani.

Nimekuwa nikishangazwa sana na maneno ya baadhi ya jamii eti katika
vilinge vya kahawa huwa hakuna jipya zaidi ya wapika majungu tu.

Nyamweru alifanya mahojiano na mwandishi wa makala hii na kusema
anachukizwa sana kusikia baadhi ya watu wakidai kuwa vilinge vya
kahawa ni sehemu ya wapika majungu na uongo.

Alisema kauli hiyo ni mawazo potofu na mgando kwani biashara hiyo
imekuwa ikimuingizia fedha za kuendesha maisha na zaidi anasomesha
watoto wake.

‘‘Nimekuwa nikijipatia mahitaji mengi kwa kuuza kahawa hii na maisha
na familia yangu yanakwenda vizuri sasa nashangzwa na watu wasiokuwa
na staha na kazi za watu inanikera mno kusikia kahawa ni sehemu ya
wabishi na wapika majungu na umbea.” Alisema.

Nyamweru ambaye ni mwenyeji wa toka mkoa wa Kigoma,ameongeza kuwa
licha ya biashara hiyo kudharauliwa na watu eti ni kijiwe cha majungu
na kujadili watu,anasema amekuwa akilipa ushuru wa sh 5,000 kwa
maofisa wa halmashauri ya manispaa Tabora na hiyo inathibitisha kuwa
biashara yake ina thamani licha ya wachache kuidharau.

Nyamweru mwenye mke na watoto 4 anasema anaishi maisha yenye furaha
wakati wote na anaamini kuwa biashara yake ya kuuza kahawa ni sawa na
biashara nyingine japokuwa hawathaminiwi kama na wao ni wazalishaji na
wanaendesha kaya zao.

Alisema kuwa ameoa na ana watoto wanne ambao wawili wako katika elimu
ya sekondari na wawili elimu msingi

Alisema ifikie mahali nao watambulike kama wajasiliamali kama wengine
japokuwa hawathaminiwi na kuwezeshwa kupata mikopo midogo midogo.

Alisema upo ushahidi mkubwa kuwa vilinge vya kahawa wanywaji wamekuwa
wakijadiliana mambo ya msingi sana na wana ufahamu mkubwa sana
kuhusiana na mambo ya nchi hii.

Aidha anabainisha kuwa katika kilinge chake cha kahawa wamekuwa
wakijadiliana mambo mengi yakiwemo ya dini,siasa,utamaduni,biashara.

‘‘Kama unavyoona hapa kuna watu wamekuja na vitabu vya
dini....tunajadiliana hapa mambo ya msingi na kuelimishana
zaidi.’’aliongeza.

Aidha alisema hata katika utoaji wa maoni ya katiba mpya wana imani
wakitembelewa katika kilinge chake wana mawazo mazuri sana ya kutoa
maoni hayo kwa ufasaha mkubwa.

Alisema licha ya kuuza kahawa amekuwa aliwahi kujishughulisha na
baishara za kuuza dagaa toka mkoani Mwanza.

Alisema katika bishara hiyo kuna jambo moja tu ambalo kamwe
hatalisahau maishani mwake ambalo ni la kuzama mara mbili ziwa
Victoria.

Aidha anabainisha kuwa alizama na ktumbwi wake katika siku tofauti
lakini kwa uwezo wa mwenyezi Mungu alinusurikana kifo.

‘‘Nilichungulia kifo mara mbili baada ya mtumbwi niliokuwa nimepanda
kuzama ziwa victoria.....lakini nilinusurika nikaogelea nikatoka na
hiyo ni katika kutafuta maisha.’’alisema

Anafafanua kuwa alikuwa akichukua dagaa hao toka visiwa vya Ukawa,
Kwavu, Ilugwa, Burubi,Uzinza,Ziragula,Yozo,na chamagati.

Aliongeza kuwa anaishi maisha sawa na wengine wenye kazi maofisini na
zaidi licha ya kuwa na familia anayoilea kwa kuipatia mahitaji yote
muhimu,pia amejenga nyumba yake.

‘‘Ninaishi katika nyumba yangu japokuwa ujenzi wake haukutegemea
kahawa pekee bali hata biashara ya dagaa toka mkoani Mwanza, pia
najishughulisha na kilimo pia....na haya ni sehemu ya mafanikio na
wale wanaodai kahawa ni sehemu ya wapika majungu aache tabia hiyo.’’
Alisema.

Alisema kauli ya kusema katika vijiwe vya kahawa kuna majungu na fitna
siyo kweli kwani mbona baadhi ya maofisi na idara za serikali huwa
tunashuhudia majungu na mizwengwe mingi.

Anafafanua zaidi kuwa ofisi hizo baadhi zimegeuka vijiwe vya soga huku
mara kadhaa utakuta wahusika wanapiga soga na nje kuna foleni ya
wateja ama wananchi wanaohitaji huduma za serikali.

Ifikie mahali baadhi ya biashara hasa wauzaji wa kahawa wathaminiwe
kama wafanyabiashara wengine kwani wanalipa ushuru wa masoko na hiyo
ni kazi kama kazi nyingine tu

Na anasema anashawishika kutamka kuwa ajira ya mwenyezi Mungu,haiko
katika elimu ya utawala.....bali ipo katika kile alichoandaa Mungu ili
kila mtu aishi maisha bora.

No comments: