Pages

KAPIPI TV

Wednesday, June 20, 2012

WAWILI MBARONI KWA WIZI WA NG'OMBE DODOMA

 
Na. Luppy Kung’alo  wa Jeshi la Polisi Dodoma.
 
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuiba Ng’ombe Jike mali ya Bw. JULIUS S/O MATHIAS mwenye umri wa miaka 32, Mkulima na  Mkazi wa Kijiji cha Michese.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. ZELOTHE STEPHEN alisema Tukio hilo lilitokea mnamo  tarehe 09/06/2012 majira ya saa kumi na moja (17:00 hrs) jioni  maeneo ya Kijiji cha Michese, Kata ya Mkonze Manispaa ya Dodoma.
 
Akizungumzia tukio hilo Kamanda Zelothe alisema toka Kuibwa kwa Ng,ombe huyo mlalamikaji hakuweza kutoa taarifa kituo cha Polisi na badala yake aliendelea kumtafuta katika mazizi ya wenzake hapo kijijini mpaka siku ya jumapili alipompata ndipo akatoa taarifa.
 
“Mlalamikaji anadai aligundua kuibwa kwa Ng’ombe wake huyo wakati wakiwa wanarudi toka machungoni na alipokuwa akiwahesabu ili kuwahakiki ndipo akagundua kutokuwepo kwa Ng’ombe wake huyo mwenye rangi ya kijivu.” Alisistiza Bw. Zelothe Stephen.
 
Kamanda Zelothe alisema juhudi za kumtafuta Ng’ombe huyo zilifanyika kwa ushirikiano  wa pamoja wa mlalamikaji na wanakijiji wa eneo hilo bila kutoa taarifa Polisi  na walitafuta katika mazizi yote pale kijijini lakini hawakufanikiwa.
 
 
Aidha alisema  siku ya Jumapili ya  tarehe 17/02/2012 majira ya saa kumi na mbili asubuhi alimuagiza mdogo wake aliyejulikana kwa jina la JOSEPH S/O MATHIAS kuendelea kufuatilia, akiwa katika ufuatiliaji akakutana na  mtuhumiwa aliyejulikana kwa jina la MOSES S/O MDOE mwenye umri wa miaka 20, Mkulima, Mkazi wa Michese akiwa anamswaga Ng’ombe huyo kuelekea kijiji cha Chiikwi.
 
“Alipomuuliza kulikoni anamswaga Ng’ombe huyo kuelekea kijiji cha Chiikwi, mtuhumiwa huyo alijibu kwamba amemnunua  Ng’ombe huyo toka kwa mtuhumiwa wa pili aliyejulikana kwa jina la  COSMAS S/O JUSTINE mwenye umri wa miaka 24,  Mkazi wa Michese ambaye walikuwa wote wakati huo.”aliongeza Kamanda Zelothe
 
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma alisema hali hiyo ilipelekea  wanakijiji hicho kukusanyika na kuanza kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashushia Kipigo watuhumiwa hao, lakini Raia wema waliwahi kutoa taarifa Polisi ambao walifika mapema kuwaokoa na kipigo kisha  kuwakamata.
 
Kamanda Zelothe Stephen alitoa wito  kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia dhana ya ukamataji salama na  kutoa taarifa mapema katika vituo vya Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe.
 
Bw. Zelothe alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa katika kituo cha Polisi kati katika Manispaa ya Dodoma na watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili

No comments: