Pages

KAPIPI TV

Tuesday, June 19, 2012

WAPINZANI WAIBOMOA BAJETI YA 2012/13"Zitto adai hatuwezi kukopa kulipana POSHO"



ZITTO ADAI HATUWEZI KUKOPA KULIPANA POSHO
 
KAMBI ya Upinzani Bungeni kupitia kwa Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, imependekeza bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2012/13, isijadiliwe bungeni, badala yake iondolewe ili ikatayarishwe upya.
 
Katika msimamo wao mzito bungeni jana mjini hapa, walidai kuwa bajeti ya serikali kwa mwaka ujao ina upungufu mkubwa wa mambo ya msingi yaliyokubaliwa na kupitishwa na Bunge lililopita.
 
Akiwasilisha bajeti mbadala ya kambi hiyo inayoundwa na CHADEMA, Zitto alisema Bunge haliwezi kuipokea bajeti ya serikali iliyosomwa na Waziri wa Fedha, William Mgimwa, wiki iliyopita kwani haikutenga fedha zozote za mpango wa maendeleo wa miaka mitano kama ilivyokubaliwa na Bunge.
 
Zitto alisema kuwa Bunge lilikubali kuwa serikali itenge kiasi cha sh trilioni nane kila mwaka kwa ajili ya mpango huo uliozinduliwa kwa mbwembwe na Rais Jakaya Kikwete, lakini katika hali ya kushangaza hakuna fedha zozote zilizotengwa.
“Serikali imeshindwa kuheshimu uamuzi uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya 
 
Jamhuri ya Muungano….imeshindwa kusimamia ahadi zake yenyewe, hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iiondoe bungeni, bajeti iliyoileta ili ikatayarishwe upya ikidhi matakwa ya mpango huo kama ulivyoidhinishwa na Bunge,” amesema Zitto.
 
Deni la taifa
 
Kuhusu deni la taifa, Zitto alisema hawawezi kukubaliana na bajeti iliyosheheni uzito mkubwa wa deni la taifa ambalo kwa kila dalili haliwezi kulipika na hawako tayari kuiacha serikali iendelee kukopa bila mpango na hivyo kuliweka taifa rehani.
 
Alidai kuwa kama serikali ingekopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii kama zinavyofanya nchi nyingi zilizoendelea, wasingekuwa na pingamizi, lakini wanashindwa kukubali kwa vile sehemu kubwa ya mkopo wa fedha hizo zinalenga katika matumizi ya kawaida ya serikali.
 
Kambi hiyo ya upinzani ilisema kuwa deni hilo halilipiki na ndio maana hata serikali yenyewe inajichanganya katika kuelekeza malipo ya deni hilo.
 
“Wakati serikali ikidai kuwa deni hilo linalipika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya kukua kwa deni la taifa.
 
Taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa serikali inaonyesha kuwa deni la taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka sh trilioni 10.5 kwa mwaka 2009/2010 hadi sh trilioni 14.4 kwa mwaka 2010/2011. Ukisoma taarifa ya Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, deni la taifa sasa limefikia sh trilioni 22,” alisema.
 
Alisema kutokana na serikali kukiri kuwa itakusanya mapato kidogo ya sh trilioni 8.7 kama makusanyo ya ndani huku ikitumia sh trilioni 10.6 kama matumizi ya kawaida, ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo ya nje itatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya ndani.
 
“Hatutaki mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari ya kifahari. Hatuwezi kukubali serikali iwaishi wazee wetu kwa kuwafanya waishi maisha magumu, na kizazi cha sasa ambacho kinapigika; na ikope maisha ya watoto wetu ili baadaye waje walipe madeni kutokana na uzembe wa kizazi cha sasa!” alisema Zitto.
 
Matumizi ya mwaka jana
 
Waziri huyo kivuli, alieleza sababu nyingine ya utata wa bajeti ya mwaka huu ni kutofahamika hasa fedha zilizotolewa na kuidhinishwa na Bunge kwa baadhi ya wizara zilivyofanya kazi.
 
Zitto alisema Wizara ya Miundombinu na ile ya Uchukuzi ilitengewa fedha katika bajeti iliyopita, lakini hadi sasa haijulikani zilitumikaje kwa kuwa makandarasi wanadai malipo hayo, na kibaya zaidi fedha kwa ajili ya reli hazikutolewa zote kama zilivyoidhinishwa na Bunge.
 
Alisema wizara nyingi hazikupewa fedha za maendeleo kama zilivyoidhinishwa na Bunge, huku halmashauri za wilaya zikiwa zimeathirika vibaya, ambapo ni asilimia 47 tu ya fedha zilipelekwa katika halmashauri, miji na manispaa.
 
Alisema ndio maana baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge zilikataa makadirio ya wizara kadhaa, kama vile Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Uchukuzi na ile ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
 
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla Bunge lako halijajadili makadirio ya matumizi kwa mwaka unaokuja, ni vema serikali itueleze kwanza fedha zilizotengwa mwaka uliopita na hazikufika hatima yake nini,” alihoji.
 
Vipaumbele vyao
 
Zitto alitangaza bajeti mbadala aliyoiita ya ukombozi, akisema namba moja ni kujenga mazingira ya ukuaji wa uchumi vijijini kwa kurekebisha miundomnbinu ya umeme, barabara, maji na miundombinu ya umwagiliaji.
 
Ili kutimiza hilo, walipendekeza kutumia sh bilioni 600 kila mwaka, na fedha hizo zitasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo Vijijini itakayokuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
 
Pili ni kukarabati Reli ya Kati na matawi yake ya Tanga/Arusha na Mpanda, ambapo watatenga sh bilioni 443, lengo likiwa ni kuhakikisha reli ya kati inasafirisha tani milioni 1.5 ya bidhaa kwa mwaka ambazo zitaliingizia taifa fedha za kigeni kiasi cha dola za Kimarekani 1.5 bilioni, badala ya dola 0.5 bilioni za sasa.
 
Vipaumbele vingine ni afya, elimu kwa shule na zahanati vijijini kwa kutoa motisha kwa walimu, madaktari na manesi kwa nusu ya mishahara yao. Aidha wataongeza mishahara ya walimu na manesi kwa asilimia 50 pamoja na kuboresha stahiki zao.
 
Kuongeza kima cha chini cha mshahara hadi sh 315,000 kwa mwezi, kuanzisha pesheni kwa wazee wa umri wa kuanzia miaka 60, kujenga uwezo wa viwanda vya ndani, kupunguza mzigo wa matumizi ya magari ya kifahari ya serikali kwa kuyapiga mnada, kufuta posho za vikao na kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara ili kuzalisha wataalamu katika sekta ya nishati.
 
Vipaumbele vingine ni kupunguza safari za viongozi nje ya nchi na ukubwa wa maafisa katika misafara ambayo imekuwa ikiigharimu serikali kiasi kikubwa cha fedha.
 
Vingine kupunguza misamaha ya kodi kutoka asilimia tatu hadi moja ya pato la taifa, kuboresha kodi katika sekta ya madini ili taifa lipate asilimia 25 ya mauzo yake, kushusha kiwango cha kodi ya wafanyakazi (PAYE) kutoka asilimia 14 ya sasa hadi 9 ili kupunguza makali ya maisha kwa mfanyakazi.
 
Kamati ya Fedha na Uchumi
 
Mapema akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Mwenyekiti wake, Andrew Chenge, aligusia kuwa mfumko mkubwa wa bei za bidhaa ambao umeongezeka kufikia asilimia 19.8 katika kipindi cha Desemba 2011, kutoka asilimia 5.6 Desemba 2010, ni jambo la hatari kwa maendeleo ya taifa.
 
Alisema hadi kufikia Aprili, 2012 mfumko wa bei ulikuwa asilimia 18.7 ambao ulisababishwa na kupanda kwa bei ya vyakula na hasa mchele, unga wa sembe, mafuta ya kula na sukari.
Sababu nyingine ni kupanda kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia, gharama ya nishati ya umeme pamoja na kuongezeka kwa gharama ya uzalishaji wa bidhaa muhimu za viwandani na usafirishaji.
 
Chenge alisema ingawa serikali ilijaribu kudhibiti kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, bado kuna changamoto kubwa katika kumpunguzia mwananchi makali ya maisha.
 
Aidha thamani ya sh ya Tanzania dhidi ya dola ya Kimarekani ilishuka kufikia dola 1599.98 katika kipindi cha mwaka 2011 kutoka dola 1449.5 kwa kipindi cha mwaka 2010.
 
Kwa upande wa sekta ya kilimo kamati hiyo imeitaka serikali ichukue uamuzi wa makusudi na kuweka vivutio katika kilimo vitakavyogusa wakulima wote nchini ili wazalishe zaidi ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika mabonde mengine yaliyo katika ukanda wa ziwa na maeneo mengine nchini.

No comments: