Pages

KAPIPI TV

Thursday, June 14, 2012

POLISI SERENGETI ADAIWA KUUA RAIA KWA KUMCHOMA SINGE AKIMTUHUMU KWA UWINDAJI HARAMU WANYAMAPORI “Uchunguzi ulibaini utumbo mpana umepasuka,Polisi aliyehusika ahamishwa Kituo cha Kazi"



Na Anthony Mayunga-Serengeti
Juni 14,2012.

WIMBI la polisi kuua raia limeendelea kushika kasi ambapo safari hii askari wa kituo kidogo cha Ikoma robanda wilayani Serengeti anatuhumiwa kumchoma kwa singer ya bunduki mtuhumiwa wa ujangili na kupasua utumbo mkubwa na kusababisha kifo chake.
 
Tukio hilo linalodaiwa kuwa la tano toka mwaka jana kufanywa na polisi wilayani hapa limethibitishwa na polisi na uongozi wa hospitali teule ya Nyerere ddh linadaiwa kutokea juni 8 kijijini Ikoma robanda.
 
Akiongea na Mwandishi wa habari hizi mbele ya Mwenyekiti wa wasaidizi wa Sheria na Haki za Binadamu wilaya Samwel Mewama kwa shida muda mfupi kabla ya kukata roho akiwa hospitalini alikokuwa amelazwa Jumanne Samson(35)mkazi wa kijiji cha Burunga alisema alichomwa na askari polisi aliyemtaja kwa jina moja la Pius.
 
Akiongea kwa vituo na kwasauti ya mbali alisema wakiwa wanakunywa pombe kijijini hapo alipokwenda kuwaona wadogo zake,”tukiwa wengi tunakunywa pombe za kienyeji majira ya saa 5,niliona mwanga  wa tochi unamulika kisha unazima nikataka kujua , ghafla nikaambiwa kaa chini “alisema.
 
Alidai hakuweza kukaa chini kwa kuwa hakuwajua waliomweka chini na wakamvamia na kuanza kumshambulia kwa mateke na magumu huku akipiga kelele kuomba msaada ,huku wakimwambia atoe nyama kwa kuwa yeye ni jangili na ghafla askari hiyo akamchoma singer chini ya kifua.
 
“Nililia sana kwa maumivu hayo,wakanikamata na kumkamata mwingine Juma Moremi ambaye tulikuwa tunakunywa naye na kutupiga kisha wakatupeleka mahabusu ya polisi wakidai wameambiwa na infoma wao sisi ni majangili”alisema kisha akadai anajisikia vibaya sana.
 
Hata hivyo alidai kuwa walifikishwa polisi juni 9/2012 ambao waliwakataa kuwapokea kutokana na hali waliyokuwa nayo,na kufikishwa hospitali huku polisi wakidai kuwa amejichoma kisu na madaktari wakashindwa kumhudumia kwa wakati kwa kuwa walikuwa chini ya ulinzi.
 
Mdogo wake anena.
Nyangi Samson(30)mdogo wake ambaye ni mfanya biashara wa maji na chakula kijijini hapo alisema kuwa kaka yake alifika juni 8,2012 kwa ajili kutafutiwa kazi yaulinzi na juni 9 ,asubuhi alipokea taarifa ya kaka yake kupigwa na kuumizwa na polisi waliokuwa wakishirikiana na askari wa hifadhi ya taifa ya Serengeti.
 
“Tulienda na mwenyekiti wa kitongoji cha senta John Kisiroti  hadi polisi,kwa kweli tulimkuta akiwa katika hali mbaya zaidi akilalamika kuchomwa singer na hali yake ni mbaya,hata hivyo polisi hasa huyo Pius alikuwa akidai anajifanya ni mzima”alisema kwa uchungu.
 
Alisema alipomuuliza polisi Pius sababu za kumuumiza kaka yake wakati amewakuta kwenye kinywaji ,alijibu kwa jeuri”wewe ulitaka mimi aniumize,huyu hajaumia anajifanya na kama ameumia basi mahakamani ataeleza “alimjibu huku akimpiga piga  Samson ambaye sasa ni marehemu.
 
Alidai baada ya kuchachamaa kwa kaimu mkuu wa kituo aliyemtaja kwa jina moja la koplo Chadel mwisho wakawapeleka hospitali kwa matibabu kwa kuwa wote wawili walionekana kulalamika kuumizwa.
 
Hata hivyo juni 10 alipofika hospitali alimkuta mama yake Rhobi Mang’ombe akiwa na mdogo wake Motondi Samson  wakiwa nje kwa kuwa polisi hawakutaka ndugu wasogee huku polisi wakitoa taarifa hospitalini hapo kuwa mtuhumiwa huyo hana ndugu.
 
“Niliomba kumwona na kumpa hata soda kwa kuwa toka juni 8 walipomkamata hakuwa amepata chakula,wala matibabu,polisi waliokuwa kwenye ulinzi walinifukuza nisimpe soda,kwa kweli walimfanyia unyama sana kaka yangu”alisema akitokwa na machozi.
 
Madai yaliyoungwa mkono na mmoja wa ndugu wa marehemu Barnabas Maro ambaye ni mkuu wa gereza mstaafu ambaye alidai kuwa waganga walichelewa kutoa huduma kutokana na jinsi polisi walivyopotosha ukweli wa tukio hilo.
 
Msimamo huo wa polisi waliokuwa wakiwalinda hawakutaka Shuhuda.
 
Mmoja wa mashuhuda wa tukio ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kuwa polisi huyo ambaye inadaiwa alichukua bunduki kituoni bila kuandika anaenda wapi na kufanya nini aliwataarifu askari wa Senapa kuwepo kwa majangili na walipofika walivamia bila kuwa na uhakika kati ya hao walikuwa wakinywa pombe yupi ni jangili.
 
“Inaonekana taarifa wanazopewa na infoma ambao wanalipwa kwa kutoa taarifa nyingi ni za uongo,na askari polisi wengi hasa huyo waki kifedha zaidi hivyo waliamini kuwa kwenye kundi hilo wangepata chochote,uchunguzi wa kina ufanyike zaidi kwa kuwa askari wa Senapa hawafanyi doria kwenye makazi ya watu lazima waongozwe na polisi”alisema.

Majeruhi mwingine anena.
Juma Moremi(45)mkazi wa kijiji cha Miseke aliyelazwa kitanda namba 15 wodi ya wanaume akiwa na pingu mkononi alisema alivamiwa na askari wakati amelala na kumkamata kisha kuanza kumpiga wakimtaka aeleze zilipo nyama pori.
 
Alidai alipigwa na kitako cha bunduki sehemu ya kiuno na sasa anakojoa damu ,huku  huduma anazopata zikiwa za kusua sua,kwa kuwa ndugu zake hawaruhusiwi kwenda kumwona na kumhudumia.
 
Uchunguzi wafanyika.
Uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanywa na daktari Safina Mussa chini ya Inspekta wa polisi Abdallah  Idd ,mwanasheria wa Senapa Msei na ndugu wamarehemu ulibaini kuwa utumbo mpana ulipasuliwa na singer hiyo na kusababisha mfumo mzima wa chakula kutokufanya kazi.
 
Kutokana na hali hiyo hakuwa na uwezo hata wa kujisaidia na hata figo inadaiwa zilishindwa kufanya kazi na ndiyo sababu hata madaktari walishindwa kumfanyia upasuaji kwa kuwa alichelewa kupata huduma.
 
Polisi ahamishwa .
Habari za uhakika zilizotufikia  muda mfupi kabla ya kwenda hewani askari anayetuhumiwa na mauaji hayo amehamishiwa kituo kikuu cha polisi Mugumu,hatua ambayo imetafsriwa kuwa askari wote waliohusika na mauaji wilayani hapa walitunukiwa uhamisho.
 
Polisi wameahidi kutoa kauli juu ya tukio hilo,kamanda wa polisi mkoa wa Mara Absolom Mwakyoma kwa muda mrefu alikuwa kwenye kikao huku
kamanda wa upelelezi mkoa aliyeko kwenye eneo la tukio alidai kuwa yeye si msemaji .
Inaendelea.

No comments: