Pages

KAPIPI TV

Friday, June 29, 2012

EGPAF YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KWENDA VIJIJINI KUANDIKA HABARI ZA UKIMWI

 Afisa program PMTCT & CT wa EGPAF Dr.Tresphory Rugagura  na Afisa uhamasishaji  EGPAF Dar-es-Salaam Bi.Mercy Kayanda wakati wakizungumza na waandishi wa habari mkoani Tabora.
 Maafisa wa EGPAF
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa na Maafisa wa EGPAF katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za EGPAF Tabora mjini.

Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na mpango wa kuzuia maambukizi VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto la EGPAF limewataka waandishi wa habari kwenda vijijini kuandika habari zinazohusu Ukimwi hatua ambayo itasaidia katika kampeni ya kupambana na janga hilo.

Akizungumza na baadhi ya waandishi hao katika ofisi za EGPAF mjini Tabora,Afisa Program ya PMTCT wa Shirika hilo Dr.Tresphory Rugagura alisema ipo haja kwa jamii kupata habari zinazohusu maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na hivyo kuwataka waandishi  wa habari kufanya hivyo kwani wanao mchango mkubwa katika kuielimisha jamii.

Akielezea mafanikio yaliyofikiwa na EGPAF tangu mwaka 2003 hadi machi mwaka huu,shirika hilo limewezesha kinamama wapatao 1,827,052 kupewa ushauri nasaha  ambapo kati yao 75,383 ambayo ni sawa na asilimia 4.1 walikuwa na virusi vya Ukimwi na huku 65,810 ikiwa ni asilimia 87.3 walipatiwa kinga ya kuzuia maambukizi kwa mtoto.

Dr.Tresphory alibainisha kuwa watoto wapatao 31,932 waalipatiwa kinga ya kuzuia maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa mama ambayo pia ni sawa na asilimia 42.3

Sambamba na hilo EGPAF tangu mwaka huo wa 2003 hadi machi 2012 imewezesha uandikishwaji wa watu waishio na virusi vya Ukimwi mkoani Tabora wapatao 177,298 wakiwemo watoto 15,007 walio chini ya umri wa miaka 15 katika vituo vya tiba ambapo miongoni mwao 94,057 wakiwemo watoto 8652 chini ya umri wa miaka 15 walianzishiwa dawa ya kufubaza makali ya virusi vya ukimwi.

Kwaupande mwingine Dr.Tresphory aliwaeleza waandishi wa habari kuwa zaidi ya bilioni mbili fedha za kitanzania zimetolewa kutekeleza miradi ya Ukimwi kwa mkoa wa Tabora katika kipindi cha mwaka 2012/2013.

Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo Dr.Tresphory akawataka waandishi hao wa vyombo mbalimbali vya habari kuihamasisha jamii hasa wanaume kuona umuhimu wa kuwasindikiza wake zao kliniki wakati wakiwa wajawazito.    


No comments: