Pages

KAPIPI TV

Wednesday, May 16, 2012

WACHUNGAJI WAILALAMIKIA SERIKALI KUKITHIRI KWA VITENDO VYA MAUAJI TABORA

 Mwili wa marehemu Mzee Obed Sikawa wakati ukiagwa katika kanisa la KKKT Tabora mjini,ambapo imeelezwa kuwa aliuawa kwa kupigwa kwa fimbo  na majambazi Jumatatu 14 Mei 2012 katika barabara ya Sikonge eneo la mto Wala.
 Baadhi ya viongozi wa dini ya kikristo wakiaga mwili wa marehemu Sikawa katika kanisa la KKKT Tabora mjini
   Waombolezaji wakiwemo ndugu na jamaa wa marehemu wakati wa kuagwa kwa mwili huo ambao umesafirishwa leo kuelekea Arusha nyumbani kwao marehemu kwa ajili ya mazishi.
 Mratibu na kiongozi wa mradi wa vijiji vya Milenia Mbola Dk.Gerson Nyadzi akiwa ni mmoja wa waombolezaji katika msiba huo.
 Mchungaji Peter Ezekiel wa KKKT Tabora wakiwa na Mchungaji Elias Mbagatta wa kanisa la Injili Afrika mkoani Tabora wakiwa katika msiba huo mara baada ya kukamilisha Ibada ya sara ya kuuaga mwili..
 Baadhi ya waombolezaji wakiwa na nyuso za majonzi wakiwa nje ya kanisa la KKKT Tabora wakati wa kuaga.
 Wachungaji wa makanisa mbalimbali ya mjini Tabora waliohudhuria shughuli ya kuuaga mwili wa marehemu Obed Sikawa katika kanisa la KKKT Tabora mjini.

Na mwandishi wetu Tabora
Mchungaji mteule wa kanisa la KKKT Tabora mjini Patrick Kiula ameitaka serikali kufuatilia na kushughulikia haraka vitendo vya mauaji ambavyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara mkoani Tabora na kusababisha vifo vingi visivyo vya lazima kwa raia wema.

Akizungumza katika  ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Mzee Obed Sikawa aliyeuawa kwa kupigwa fimbo kichwani na majambazi jumatatu wiki hii katika barabara ya Sikonge eneo la mto Wala wakati akitokea shambani kwake,Mchungaji Kiula alisema vitendo vya mauaji kwa mkoa wa Tabora kwasasa vimekithiri na hivyo wao kama kanisa linawajibu wa kuikemea Serikali kushughulikia kwa haraka kwani idadi kubwa ya watu wamekuwa wakipoteza maisha na hawaoni hatua zozote zinazochukuliwa dhidi matukio ya aina hiyo.

Aidha Mchungaji Kiula alisema mbele ya mamia ya waombolezaji waliofurika katika kanisa la KKKT Tabora kuwa kitendo cha serikali kukaa kimya kutokana na matukio hayo ya kinyama kimekuwa kinatafsiri tofauti mbele ya wananchi wake ambao ndio waathirika wakubwa wa matukio hayo.

''Sisi kama kanisa hatuwezi kukaa kimya kuona wananchi kila kukicha hapa Tabora wanauawa pasipo hatia,halafu serikali inatambua na pengine hata baadhi ya watendaji serikalini wanawatambua wauaji,wanawaacha tu,watu wanaendelea kupoteza maisha na mali zao na wengine wanasababishia ulemavu wa kudumu....kwakweli hapana tunataka serikali ishughulikie suala hilo"alisema mchungaji Kiula huku vilio na sauti ya waumini na waombolezaji waliokuwa wakimsikiliza vilisikika katika kanisa hilo.

Kauli hiyo ya mchungaji Kiula imeungwa mkono pia na wachungaji wengine waliohudhuria ibada hiyo akiwemo mchungaji wa kanisa la Injili Afrika Elias Mbagatta lililopo eneo la Mwanza road mjini Tabora. 

Marehemu Mzee Obed Sikawa inadaiwa kuwa wakati akitokea shambani kwake barabara ya Sikonge majira ya jioni,akiwa amepanda pikipiki akiwa na mwenzake,ghafla walikuta kamba imetegwa njiani iliyowafanya waanguke na mara baada ya kuanguka,kikundi cha watu kilifika na kuanza kuwashambulia ambapo marehemu alipigwa fimbo kichwani iliyosababisha kifo chake muda mfupi mara baada ya kufikishwa Hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete.

Habari kutoka kwa ndugu na jamaa wa karibu zinasema kuwa marehemu baada ya kuanguka waharifu hao walimpokonya simu yake ya kiganjani na fedha taslimu kiasi cha shilingi elfu hamsini.

Aidha matukio ya mauaji kwa kutegewa kamba kwa waendesha pikipiki hapa mkoani Tabora yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kuhofisha maisha ya watu na mali zao.   

  



No comments: