Pages

KAPIPI TV

Tuesday, April 17, 2012

ZOEZI LA UKAGUZI WA MIPAKA KATIKA MAANDALIZI YA SENSA YA WATU NA MAKAZI LAENDELEA




Mkurugenzi mkuu ofisi ya Taifa ya Takwimu Dr.Albina  Chuwa amesema tatizo la rasilimali fedha linalokabili zoezi la utoaji wa hamasa kwa wananchi kuhusu elimu ya umuhimu wa Sensa ya watu na makazi halitaathiri ufanikishwaji wa zoezi hilo.

Dr.Chuwa aliyasema hayo wakati  akiwa na timu ya wataalam kutoka ofisi ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati walipokuwa wakikagua maandalizi ya zoezi la Sensa ya watu na makazi katika wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Wakiwa wilayani Nzega baada ya kukamilisha katika wilaya za Uyui na Tabora Manispaa timu ya wataalamu hao ilitembelea maeneo yaliyopimwa na kuandaliwa katika ramani ili kuwezesha zoezi hilo la kuhesabu watu na makazi kufanyika kwa uhakika ifikapo tarehe 26 Agosti mwaka 2012.

Hata hivyo pamoja na kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha katika utoaji wa hamasa kwa wananchi kutambua umuhimu wa zoezi hilo ambalo kimsingi linasaidia Serikali katika kuwahudumia wananchi wake,Mkurugenzi huyo Dr.Chuwa amezihimiza Halmashauri kutumia fursa zilizopo ili kukamilisha mchakato huo.

Kwaupande mwingine Kamishna wa Sensa  Hajjat Amina Mrisho Said alitoa rai kwa halmashauri ya Nzega kutumia vyombo vya habari vya ndani ya wilaya hiyo kama Televisheni na Redio kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kuhusu umuhimu wa Sensa ya watu na makazi.



No comments: