Jeshi la Polisi mkoani Tabora limefanikiwa kukamata bunduki aina ya Shortgun Greener baada ya kuwakurupusha majambazi wanaodaiwa kuwa walikuwa wametoka kufanya uharifu katika ofisi za kampuni ya ulinzi ya Kitumbo ya mjini Tabora.
Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora ACP Anthony Rutha katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema askari sita wa jeshi hilo manispaa ya Tabora wakiwa katika doria,waliwaona watu wawili waliokuwa wakiendesha baiskeli mbili huku wamebeba mizigo katika baiskeli hizo waliwatilia shaka na kuwataka wasimame lakini watu hao walitupa mizigo waliyokuwa nayo na kuanza kutimua mbio.
Askari hao wakiongozwa na Inspekta Langoma,baada ya watu hao wanaodaiwa kuwa ni majambazi kutupa mizigo hiyo,askari waliamua kuipekua na kukuta bunduki hiyo Shortgun Greener yenye nambari R 53472 na vifaa mbalimbali vya ofisini.
Kamanda Rutha alisema baada ya upelelezi kufanyika ilibainika kuwa majambazi hayo yalikuwa yametoka kuvamia ofisi ya Kitumbo Security na kufanikiwa kuiba vitu hivyo.
Aidha kwa upande mwingine kamanda Rutha amewataka raia wema kulisaidia jeshi hilo kwa kuwabaini watu hao na kutoa taarifa kwa jeshi hilo.
No comments:
Post a Comment