Baadhi
ya wanakijiji wa kijiji cha Kabita wilayani Busega, Simiyu wakifuatilia
mkutano wa kijiji uliokuwa ukijadili hali ya Chakula na Lishe kijijini
hapo wakati Ofisi ya Waziri Mkuu ilipofika kijijini hapo kufanya
tathmini ya masuala hayo Oktoba, 2014.
Bw.
Clement Ngosha wa kijijini Kabita Wilayani Busega, Simiyu, akitumia
mbegu za mahindi kueleza hali ya chakula kijijini hapo kwa wataalam wa
Tathmini ya Hali ya Chakula na Lishe inayofanywa na Ofisi ya Waziri
Mkuu, Oktoba, 2014.
Mtaalam
wa Usalama wa chakula kutoka Wizara ya kilimo, chakula na Ushirika, Bi.
Tatu Kayumbu akiihoji moja ya kaya kijijini Mwamanyili,Wilayani Busega,
Simiyu wakati wa Tathmini ya Hali ya Chakula na Lishe inayofanywa na
Ofisi ya Waziri Mkuu kijijini hapo, Oktoba, 2014.
……………………………………………………………….
Na. Ibrahim Hamidu
Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu wa maafa inafanya
Tathmini ya Hali ya Chakula na Lishe Mkoani Simiyu katika Wilaya zake
zote ambazo ni; Halmashauri za Wilaya za Bariadi, Itilima, Maswa
,Bariadi Meatu na Busega.
Akiongea mkoani Simiyu kiongozi wa Wataalam wa tathmini ambaye
pia ni mratibu wa shughuli za maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Edgar Senga
alibainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imefikia maamuzi hayo ya kufanya
tathmini mkoani Simiyu baada ya mkoa huo kutuma maombi katika Ofisi hiyo
kuwa wana upungufu wa chakula.
“ Ofisi ya mkoa ya Simiyu ilileta maombi kwa ofisi ya Waziri
Mkuu kuwa wanaoupungufu wa chakula takribani tani 48,975, kwa kuwa Ofisi
yetu ndio yenye dhamana ya kuratibu misaada ya chakula hivyo
haikuwanabudi kufanya tathmini ya haraka ili kubaini hali ya chakula ya
mkoa huu ili kuweza kuamua namna ya kushughulikia maombi yao ya msaada
wa chakula” alisema Senga
Senga alibainisha kuwa Wataalam wa tathimini hiyo wanatoka
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika Idara ya Usalama wa Chakula
ambao kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wametawanyika katika
Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu ambapo katika kila Wilaya vitachaguliwa
vijiji vitatu vya kufanyiwa tathmini.
“Katika kila kijiji wataalamu hawa watakuwa wanamadodoso ya
Wilaya na kijiji ambayo yatasaidia kutoa taarifa mahsusi za hali ya
chakula na Lishe katika ngazi ya Wilaya na Kijiji, lakini pia wataalamu
wanayo madodoso ya kaya ambayo yanalenga kupata taarifa za hali ya
chakula na Lishe kwa kaya husika kwa vijiji vitakavyoteuliwa na Serikali
za vijiji hivyo. Kwa kuzingatia kuwa wataalam wa masual ya chakula
katika ngazi ya Wilaya watakuwa wanahusishwa ninaamini tutapata taarifa
bora ya hali ya chakula ya mkoa wa Simiyu ” alisisitiza Senga.
Akiongea Ofisini kwake alipotembelewa na ujumbe wa Wataalamu hao
Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) mkoani Simiyu, Bw. Joseph
Nandira alibainisha kuwa Katika kipindi cha msimu wa 2013/2014, Mkoa
ulijiwekea malengo ya kuzalisha jumla ya tani 1,003,578 za mazao ya
chakula aina ya nafaka/wanga na tani 150,257 aina ya mikunde. Mavuno
halisi yaliyopatikana ni tani 476,024 za chakula aina ya nafaka/wanga na
tani 74,944 za chakula aina ya mikunde.
Nandira alibainisha kuwa kutokana na tabia ya wananchi kuuza
sehemu kubwa ya chakula ili kukidhi mahitaji ya familia zao, tathmini ya
hali ya chakula tuliyoifanya mwezi Julai 2014, tulibaini kuwa Mkoa
Unaupungufu wa chakula wa tani 48,975 za nafaka ambao umeanza kuanzia
mwezi Oktoba na upungufu huo wa chakula unatarjiwa kuwepo mwezi
Novemba/Desemba hadi Februari, 2015 kama wilaya hazitapata msaada wa
chakula.
“Tathmini hiyo ilibaini Halmashauri za Wilaya za Busega na Meatu
zina upungufu wa chakula kuanzia mwezi Agosti, 2014 hadi Februari,
2015. Halmashauri za Wilaya za Bariadi, Itilima, Maswa na Bariadi Mji
zina upungufu wa chakula kuanzia mwezi Oktoba, 2014 hadi mwezi Februari,
2015. Ili kukidhi haja ya upungufu wa chakula ndio maana tuliomba jumla
ya tani 48,975 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.” Alisema Nandira
Nandira alifafanua kuwa ili kuhakikisha tatizo la upungufu wa
chakula linakwisha tayari mkoa unayomikakati ambayo inajikita katika
Kuwahimiza wananchi kutumia vizuri chakula kilichopatikana na kuepuka
matumizi yasiyo ya lazima. Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu makadirio ya
mahitaji ya chakula ngazi ya kaya kwa mwakapamoja na Kuwashauri wananchi
kuuza sehemu ya mifugo yao na kujinunulia chakula wakati huu ambapo
chakula bado kina bei ndogo na kinapatikana ndani ya Wilaya na Mkoa.
Aliongeza kuwa mkoa unaendelea
kuwashauri wananchi kujinunulia chakula kutokana na fedha za mauzo ya
pamba. Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hifadhi bora ya chakula, ikiwa ni
pamoja na matumizi ya vihenge bora/vya kisasa na madawa ili chakula
kisibunguliwe na wadudu. Kuwashauri wananchi kuuza ziada ya chakula
walichovuna na si vinginevyo.
Kwa mujibu wa sensa ya watu ya
mwaka 2012 mkoa wa Simiyu una jumla ya watu 1,584,157 ambao wanahitaji
jumla ya tani 404,752 za chakula aina ya nafaka/wanga na tani 144,553 za
chakula aina ya mikunde kwa kipindi cha msimu wa mwaka 2013/2014.