Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda, amemtaja Bosco Ntaganda kama mtu mwenye sifa mbaya.
Kesi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani wa waasi Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC inatarajiwa kuanza kesho.
Ntaganda anatuhumiwa kupanga na kuendesha kampeini ya kikatili Mashariki mwa Congo.
Bensouda amesema Ntaganda aliwalazimisha mamia ya watoto kujiunga na jeshi lake na kwamba wanajeshi wasichana walibakwa na kuwekwa kama watumwa wa ngono.
Wakili wa Ntaganda anayetoka Canada, aliambia wanahabari kuwa tangu atupwe korokoroni, Ntaganda amepunguza sana uzani wake na anawakosa watoto wake 7.
Lakini kiongozi huyo wa zamani wa kundi la waasi, anasubiri sana kujitetea kwa kutoa hotuba kortini kesho.
Zaidi ya waathiriwa 2000 wameidhinishwa kushiriki katika kesi hiyo kama mashahidi.
Upande wa mashtaka unapanga kuita wanajeshi watoto wa zamani kama mashahidi katika kesi hiyo.
Kiongozi huyo wa mashtaka alisifu Congo kwa ushirikiano wake na ICC na kutoa wito kwa waathiriwa wawe na subira, akisema, lengo moja muhimu la haki ni kufichua ukweli.
''Shughuli yenyewe huenda ikaonekana kujikokota lakini hatua zote sharti zilenge kupata ukweli'' Alisema Bensouda.
Bosco Ntaganda anakanusha mashtaka yote 18 yaliyowasilishwa dhidi yake na kesi hiyo inatarajiwa kuchukua miaka kadha.
Chanzo:-BBC Swahili
No comments:
Post a Comment