Pages

KAPIPI TV

Thursday, July 2, 2015

ZANTEL YATOA SH.MILIONI 5 KUSAIDIA CHAMA CHA MAALBINO TANZANIA KUTOA ELIMU KWA UMMA

Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Pratap Ghose (katikati) akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi kuhusu ushirikiano wao na chama cha Maalbino Tanzania. Kulia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Zantel,  Progress Chisenga, na Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimaya.
Mkurugenzi wa Masoko wa Zantel,  Progress Chisenga (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimaya (katikati), akizungumza katika mkutano huo wakati akiishukuru Zantel kwa msaada huo kwa chama hicho.
Meneja wa Chapa ya Zantel, Arnold Madale (kulia), akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu msaada huo.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Pratap Ghose(wa nne kulia),   akikabidhi mfano wa  hundi ya shilingi milioni tano kwa Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimaya (kushoto) kwa ajili kusaidia chama cha Maalbino Tanzania kutoa elimu kwa umma kuhusu changamoto walizonazo. Wengine ni maofisa kutoka chama cha Maalbino na maofisa wa Zantel.

Na Dotto Mwaibale


Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel leo imekisaidia Chama cha Maalbino Tanzania katika mpango wake wa kusambaza elimu juu ya ulemavu wa ngozi kwa jamii pamoja na msaada wa jumla ya shilingi milioni 5 ambao unalenga kusaidia uendeshaji wa shughuli zake hapa nchini.

Zantel kwa kushirikiana na Chama Cha Maalbino kitajikita kutoa elimu hii kwa kusambaza ujumbe mfupi kwa wateja wake pamoja na kutumia vipindi vyake inavyodhamini ili kupeleka ujumbe kwa jamii kiujumla.

Pamoja na hiyo pia, Zantel inajipanga kutumia mikutano ya wafanyakazi pamoja na matamasha ili kuhakikisha ujumbe kuhusu ulemavu wa ngozi unawafikia watu wengi zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, Pratap Ghose alisema mchango huo katika kuwawezesha Chama cha Maalbino ni sehemu ya huduma za kampuni yake kwa jamii.

“Tatizo kubwa ni ukosefu wa elimu miongoni mwa wanajamii, na kwa hakika hatua kubwa imepigwa katika kupambana na tatizo hili tayari, na sisi kama Zantel tunaamini kwa kutumia uwezo wetu kama kampuni ya simu tunaweza kushiriki kulimaliza tatizo hili la mauaji ya ndugu zetu’ alisema Pratap.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina jumla ya watu wenye ulemavu wa ngozi 5,200 na wengi wao wanaishi kanda ya ziwa, na toka mwaka 2009 jumla ya kesi 155 zinazohusu walemavu wa ngozi zimeripotiwa kwa vyombo vya sheria kwa mujibu wa taasisi ya Under the Same Sun.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimaya, ameipongeza kampuni ya Zantel kwa mchango wao akisema utasaidia sana katika juhudi zao za kupigania haki za walemavu wa ngozi nchini.

‘Watu wenye ulemavu wa ngozi ni kama binadamu wengine wa kawaida, hivyo tunaiomba jamii isiwatenge ndugu zetu hawa’ alisema Kimaya.

Bwana Kimaya pia aliomba wadau wengine wajitokeze kuwawezesha walemavu wa ngozi waweze kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo.


“Jamii yetu ya walemavu wa ngozi ina matatizo mbalimbali, hivyo tunazidi kuwaomba watu binafsi, serikali pamoja na makampuni mbalimbali wazidi kujitokeza kusaidia kundi hili la jamii’ alisisitiza Kimaya.

No comments: