Wananchi wakiangalia michoro ya ramani ya viwanja vyao iliyochorwa na Kampuni ya Ardhi Plan Limited |
Na Mwandishi wetu.
Wananchi zaidi ya 1144 eneo la Uledi kata ya Ipuli Manipaa
ya Tabora wamelalamikia ucheleweshwaji wa upimaji wa ardhi ya maeneo wanayoishi
hatua ambayo imewatia hofu ya kuona kuwa huenda wakaporwa maeneo hayo na baadhi
ya watendaji wachache wa kitengo cha ardhi manispaa ya Tabora.
Wakizungumza katika mkutano wa dharura ulioitishwa na kamati
ya ardhi iliyoteuliwa na wananchi hao baada ya kubaini kuwa upo uwezekano wa
kupoteza maeneo yao kufuatia halmashauri ya manispaa ya Tabora kusuasua
kuwapimia maeneo yao ambayo wanahitaji kuyaendeleza kwa ajili ya makazi,walisema
kuwa hawatakuwa tayari kuona wanapoteza haki yao ambayo itaporwa na wajanja
wachache.
Mwenyekiti wa kamati ya ardhi ya eneo hilo la Uledi Bw.Aman
Mbwambo alisema licha ya kuendelea kudai wapimiwe maeneo yao kwa zaidi ya miaka mitano na hata
kufikia hatua ya kufungua kesi mahakamani kitengo cha ardhi mwaka 2012 na
mahakama kutoa uamuzi wa kuwapa haki ya kupimiwa lakini halmashauri ya manispaa
ya Tabora bado imeshindwa kutekeleza agizo hilo la mahakama.
Mbwambo alisema baada ya
kubaini kuwepo kwa mizengwe
inayofanywa na baadhi ya watendaji wa
halmashauri ya manispaa ya
Tabora kamati yake ilipewa baraka na wakazi wa eneo hilo la Uledi
kuingia mkataba na kampuni ya Ardhi Plan Limited kupima viwanja hivyo hatua ambayo
pia iliridhiwa na baraza la Madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Tabora.
Kufuatia makubaliano yaliyofikiwa baina ya wakazi wa Uledi na Kampuni ya Ardhi
Plan Limited ya kupima viwanja hivyo ambavyo wananchi hao wanadai kuwa watanufaika
kwa kuuza kila kiwanja kimoja kati ya shilingi milioni moja hadi moja na laki tano kupitia Kampuni hiyo,huku
halmashauri ikihitaji kupima yenyewe na kufidia kila kiwanja kwa kulipa wananchi hao
shilingi laki sita,jambo ambalo
wamedai kuwa ni wizi wa mchana kweupe.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Ardhi Plan
Limited Bw.Gombo Samandito alisema kampuni yake tayari imekwisha yapima maeneo
hayo na kuyafanyia uhakiki kwa kila mwananchi ikiwa ni pamoja na kuchora ramani
ya viwanja hivyo lakini jambo la kusikitisha ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri
ya manispaa ya Tabora imeshindwa kutoa kibali cha kuruhusu taratibu zingine
kuendelea ikiwa ni pamoja na kuweka mawe ya msingi na kuanza kuchonga barabara
za mitaa kwa kufuata kanuni za mipango miji.
Hata hivyo baadhi ya wananchi katika mkutano huo wa dharura
wa kujadili hatma ya kupimiwa maeneo yao,wameonesha kushitushwa kwao na kitendo
cha watumishi wa Idara ya ardhi manispaa ya Tabora kuingia kinyemela na kuanza
kuwapimia baadhi ya watu na kuwauzia maeneo hayo jambo ambalo limeendelea
kuzidisha chuki dhidi ya wananchi hao ambao wameiomba serikali kuingilia kati
mgogoro huo.
“Jamani hivi sasa naomba tuanze kupeana taarifa ikiwa mtu
atamuona huku mtumishi wa idara ya ardhi anakuja kupima tumkamate na kumuadhibu
sisi wenyewe hata kama tutakuwa tumejichukulia sheria mkononi si vibaya kwani
tupo tayari kufa kwa ajili ya kudai haki zetu”alisema mmoja wa wananchi katika
mkutano huo.
Aidha wananchi hao wamekuwa wakifanya mikutano ya mara kwa mara kwa lengo la kujadili hatua
ya halmashauri kusuasua kuwapimia maeneo yao lakini hadi sasa hakuna taarifa
zozote zinazotolewa na ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Tabora
kuhusu mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka mitano.
No comments:
Post a Comment