BARAZA la Habari Tanzania (MCT)
limekubali kuanza ushirikiano na uhusiano mzuri na Chama cha Bloggers
Tanzania (TBN) mara kitakapo maliza mchakato wa usajili wake na
kutambulika rasmi kisheria. MCT imesema kwa hatua ya kwanza itafanya
mazungumzo na viongozi wa TBN na kujadiliana namna gani ya kuisaidia
TBN.
Kauli hiyo imetolewa juzi jijini
Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mkajanga alipokuwa
akizindiwa hafla ya kwanza ya mwaka 2015 ya wamiliki na waendeshaji wa
blogu na mitandao mingine ya kijamii iliyofanyika katika Hoteli ya
Serena.
Katibu huyo Mtendaji wa MCT
alisema kwa maendeleo ya sasa ya teknolijia ya habari na mawasiliano ni
vigumu kuzitenga blogu kama vyombo vya habari, hivyo kuahidi
kushirikiana na TBN kuhakikisha inafikia malengo yake ya kuwaunganisha
bloggers na kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili.
Alisema MCT inasubiri TBN ipate
usajili kisheria toka mamlaka husika serikalini na baada ya zoezi hilo
itaanza kushirikiana maramoja na chombo hicho kilichoanzishwa
kuwaunganisha wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya kijamii nchini na
wale wanaofanya shughuli za nje ya nchi.
“…MCT ipo tayari wakati wowote
kuanza kushirikiana nanyi kikazi, tunachosubiri ni TBN kusajiliwa
rasmi…mtakapo maliza usajili tu njooni ofisi, tutazungumza na viongozi
wenu ili kujua nini cha kuwasaidia. Naombeni msichelewe tuanze hili mara
moja,” alisema Kajubi Mkajanga akizungumza na wana-TBN kabla ya
kuzinduwa sherehe hiyo.
Awali akizungumza katika hafla
hiyo Mwenyekiti wa TBN, Joachim Mushi alisema kwa sasa mitandao ya
kijamii imekuwa ikitekemewa na kundi kubwa la jamii katika kusambaza
taarifa kwa haraka licha ya uwepo wa changamoto kadhaa ndani ya tasnia
hiyo.
Alisema pamoja na mambo mengine,
TBN imeanzishwa kwa lengo la kuwaunganisha waendeshaji na wamiliki wa
blogu pamoja na mitandao mingine ya kijamii, na pia kuhakikisha wana-TBN
wanapata fursa ya kujifunza zaidi maadili ya tasnia ya habari na
mawasiliano ili kufanya kazi zao kiufanisi zaidi.
Aidha aliishukuru Kampuni ya Simu
ya Vodacom Tanzania kwa kusaidia kufanikisha tukio la kukutana
‘bloggers’, pamoja na Benki ya NMB na makampuni mengine ya Coca Cola,
AIM Group na kampuni ya huduma za intanenti ya Raha kufanikisha tukio
hilo la kuwaleta pamoja bloggers wa Tanzania.
Akisoma risala ya wana-TBN kwa
mgeni rasmi, Mjumbe wa TBN, Henry Mdimu alisema licha ya blogu kuwa
chanzo kikubwa cha habari na mstari wa mbele kuwafikishia wananchi
habari kwa haraka zaidi lakini bado zimekuwa hazitambuliwi na mamlaka
zinazosimamia na kutetea tasnia nzima ya habari.
“…Pamoja na kazi kubwa na nzuri
inayofanywa na ‘bloggers’ na waendeshaji wa mitandao ya kijamii, bado
hawatambuliki rasmi na mamlaka husika pamoja na taasisi zinazohusika na
usimamizi wa tasnia hii likiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), Idara
ya Habari (Maelezo), MISA-Tan na hata Mfuko wa Ruzuku kwa Vyombo vya
Habari nchini (TMF).
“..Tunasema hivi maana tunaona kwa
namna moja ama ingine wadau hawa muhimu hawajumuishwi katika harakati
au michakato yoyote ile mnayoifanya kwenye tasnia hii. Mfano kupata
semina za MCT, kupewa vitambulisho (Press card), kushiriki katika
mafunzo na hata mashindano ya kila mwaka ya wanahabari yanayoandaliwa na
MCT,” alisema Mdimu akisoma risala ya TBN mbele ya mgeni rasmi Bw.
Mkajanga.
Kwa upande wa waalikwa rasmi
kutoka ubalozi wa Marekani wakizungumza katika hafla hiyo kupitia kwa
mwakilishi wao ameahidi kuisaidia TBN katika programu mbalimbali ili
kuchochea uhuru wa habari nchini Tanzania.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment