Pages

KAPIPI TV

Wednesday, October 22, 2014

"MADIWANI SIMAMIENI VIZURI MAPATO NA MIRADI YA MAENDELEO"; KAMOGA

Na Allan Ntana, Sikonge

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wametakiwa
kusimamia kwa nguvu zote ukusanyaji wa mapato ya ndani na kufuatilia
kwa karibu zaidi utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kufanikisha
shughuli zote za uendeshaji wa halmashauri hiyo kwa kiwango
kinachotakiwa.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Robert
Kamoga katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha baraza la madiwani
wa halmashauri hiyo kilichofanyika jana katika ukumbi wa Chuo cha
Maendeleo ya Jamii (FDC) mjini Sikonge.

Alisema ili halmashauri hiyo iweze kufanikisha utekelezaji wa mipango
yake ya kimaendeleo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kama ilivyopangwa
wanapaswa kuongeza juhudi katika suala zima la ukusanyaji mapato
kutoka katika vyanzo vyake vya ndani sambamba na kuwa na usimamaizi
mzuri wa mapato hayo.

Akielezea jitihada zilizowezesha halmashauri hiyo kuvuka lengo la
makusanyo katika kipindi cha msimu wa 2013/2014, alisema watendaji
wote walishikamana na kuwa kitu kimoja huku kila mmoja akitekeleza
wajibu wake ipasavyo, hivyo akawataka madiwani hao kusimamia kwa nguvu
zote ukusanyaji mapato na utekelezaji miradi ili kufanikisha malengo
ya halmashauri hiyo.

‘Waheshimiwa madiwani ili kufikia lengo la kukusanya kile
tulichojipangia hatuna budi kusimamia kwa nguvu zetu zote ili tuweze
kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maabara
kwa kila shule na shughuli zote za uendeshaji wa halmashauri yetu’,
aliongeza.

Akizungumzia mafanikio ya miradi mbalimbali ya maendeleo, Kamoga
alisema huduma katika zahanati na vituo vya afya Kitunda na Mazinge
zimeendelea kuboreshwa kwa kuongeza majengo ya upasuaji na vifaa tiba
kupitia mapato ya halmashauri na michango ya wahisani.

Huduma nyingine ambazo zimeendelea kuboreshwa ni usambazaji wa maji
safi na salama sambamba na ukamilishaji ujenzi wa miradi ya maji
Majojoro na Mibono ikiwemo mradi wa usambazaji maji Sikonge mjini,
japokuwa changamoto kadhaa zimekuwa zikijitokeza ikiwemo uharibifu wa
miundo mbinu, ukosefu wa nishati ya kuendeshea mitambo na maji
kutowafikia wananchi wote.

Aidha Kamoga alisema sekta ya elimu pia imeendelea kuboreshwa kwa
kiwango kikubwa kwa kuongeza madawati mashuleni, ujenzi wa nyumba za
waalimu na vyumba vya madarasa sambamba na uboreshaji miundo mbinu ya
barabara kwa kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya barabara zote za
vijijini na mjini.

Akitoa salaamu kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo Hanifa Selengu,
KatibuTawala wa halmashauri hiyo Geofrey Mtalemwa aliwataka watendaji
wote wa vijiji na kata kwa kushirikiana na madiwani kuhamasisha
kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika suala zima la kilimo
kwani msimu wa mvua ndio umeanza.

Pia aliwataka watendaji wote wa halmashauri, tarafa, kata na vijiji
kuhamasisha na kusimamia ipasavyo suala la elimu kwa kulipa uzito
unaostahili hasa ikizingatiwa kuwa taifa zima liko katika mchakato wa
ujenzi wa maabara katika kila shule, kwani maabara zinaendana na uwepo
wa wanafunzi, vinginevyo hatuwezi kufanikiwa.

No comments: