Na Allan Ntana, Sikonge
MTOTO Pili Ibrahimu (4) aliyezaliwa mwezi Februari
2010 katika zahanati ya Mole iliyoko katika kijiji cha Mole Kiloleli kata ya
Mole wilayani Sikonge mkoani Tabora bila kuwa na sehemu ya kutolea haja kubwa amefanyiwa
operesheni na madaktari bingwa katika hospitali ya Rufaa Bugando ili kumwezesha
kuwa na kiungo hicho muhimu katika mwili wake.
Binti huyo alifanyiwa upasuaji katika hospitali hiyo
wiki mbili zilizopita baada ya wasamaria wema kujitokeza na kutoa michango ya
fedha kiasi cha sh mil 2 ili kufanikisha safari ya kumpeleka hospitali ya Rufaa
Bugando iliyoko jijini Mwanza kwa ajili ya matibabu kama wazazi wake walivyokuwa
wameshauriwa na wataalamu wa afya.
Mafanikio ya safari na matibabu ya mtoto Pili kwa kiasi
kikubwa yalichangiwa na moyo wa huruma na jitihada za kipekee zilizofanywa na
Meneja wa shirika la Care International wilayani Sikonge Waziri Rashid Njau kwa
kushirikiana na Muuguzi wa zahanati ya kijiji hicho Bi.Deodata Raphael Lyimo
aliyetoa taarifa za kuwepo kwa mtoto mwenye tatizo hilo.
Baada ya kupata taarifa za Pili, Njau alilazimika
kusambaza taarifa za mtoto huyo katika mitandao mbalimbali ya kijamii ili
kutafuta msaada toka kwa wasamaria wema jambo ambalo liligusa watu wengi sana
ndani na nje ya mkoa wa Tabora na kuanza kutoa michango yao.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
mtoto huyo kurejea kutoka Bugando alikofanyiwa upasuaji, ‘Njau akiwa amejawa na
furaha’, alitoa shukrani zake za dhati kwa watu wote walioguswa na tatizo la
mtoto huyo na kutoa msaada uliowezesha kupelekwa Bugado kwa ajili ya upasuaji
zoezi lililofanyika kwa mafanikio makubwa.
Njau alibainisha kuwa Pili alikuwa anateseka sana
kwa sababu haja kubwa ilikuwa inatokea sehemu ya haja ndogo na kupata maumivu
makali sana kila wakati kwa kipindi chote hicho cha miaka minne jambo
lililomfanya akimbiwe na watoto wenzake na kubaki mpweke.
Akizungumzia tatizo hilo mama mzazi wa Pili, Hamisa
Masudi (35) alisema hali ya mwanae ilishamkatisha tamaa hasa ukizingatia kuwa
anaishi maisha ya umaskini sana na hakuwa na uwezo wowote wa kumpeleka kwenye
hospitali kubwa na mbaya zaidi mume wake alishamkimbia baada ya kuona
amejifungua mtoto mwenye ulemavu.
Naye Deodata Raphael Lyimo muuguzi wa zahanati ya
Mole alipongeza jitihada zilizofanywa na shirika la Care International kupitia
mradi wake wa TABASAMU ambazo zimefanikisha matibabu ya mtoto huyo na sasa
anaendelea vizuri huku akibainisha kuwa msaada zaidi bado unahitajika kwa vile
mtoto huyo anatakiwa kupelekwa tena Bugando mwezi ujao kwa ajili ya uchunguzi
wa maendeleo ya upasuaji uliofanyika.
No comments:
Post a Comment