Pages

KAPIPI TV

Sunday, August 31, 2014

WATANZANIA WAASWA KUPANDA MITI KUTUNZA MAZINGIRA


01Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akipanda mti wa pili aina ya mtiki ikiwa ni ishara ya kuthamini, kuhifadhi na kutunza mazingira nchini wakati wabunge wa bunge hilo walipotembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana mjini Bagamoyo.02Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Dkt. Margaret Zziwa akipanda mti aina ya mtiki ikiwa ni ishara ya kuthamini, kuhifadhi na kutunza mazingira nchini wakati wabunge wa bunge hilo walipotembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana mjini Bagamoyo.
……………………………………………………
Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
 
Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Dkt. Margaret Zziwa ameipa heshima Tanzania kwa kupanda mti aina ya mtiki ikiwa ni ishara ya kuthamini, kuhifadhi na kutunza mazingira nchini.
 
Spika Dkt.  Zziwa alipanda  mti huo wakati wa ziara yake pamoja na wabunge wa EALA walipotembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana mjini Bagamoyo.
 
 “Huu ni utaratibu wetu na ni azimio tuliojiwekea kama EALA kupanda miti kila tunapoenda kufanya mkutano katika nchi washirika ndani ya jumuiya yetu ili kuwasisitiza wananchi umuhimu wa kutunza mazingira” alisema Dkt.  Zziwa.
 
Dkt.  Zziwa alisema kuwa imekuwa desturi ambayo pia ni utaratibu waliojiwekea bunge hilo kupanda miti kila wanapokuwa na mkutano kila mwaka katika nchi washirika ambapo mikutano hiyo hufanyika kwa mzunguko ndani ya jumuiya.
 
Dkt. Zziwa alieleza kuwa zoezi la kupanda miti hiyo lilikuwa lifanyike Dar es Salaam lakini yeye na wabunge wa EALA waliamua lifanyike Bagamoyo ambapo pamoja na kutembelea Taasisi ya TaSUBa wamepata kujionea hazina ya historia Afrika Mashariki iliyopo katika mji mkongwe wa Bagamoyo.
 
Aidha, Dkt. Zziwa amempa jukumu la Mbunge wa EALA kutoka Tanzania ShyRose Bhanji kutembelea taasisi hiyo na kujionea hali ya miti waliyoipanda wakati wa ziara yao inavyoendelea kumea na kutoa taarifa mara kwa mara katika bunge hilo.
 
Kwa upande wake Mbunge wa EALA kutoka Tanzania Makongoro Nyerere ametoa wito kwa Watanzania wa kutunza mazingira kwa kupanda miti mingi iwezekanavyo ili kutunza mazingira.
 
Makongoro amesema kuwa ni wajibu wa kila mwananchi ahamasike, kila mwananchi mmoja mmoja apande mti mmoja autunze hadi ukue.
 
Makongoro alisisitiza kwa kusema, “Miti ina umuhimu mkubwa sana katika jamii yetu, inasaidia kutunza uso wa ardhi yetu na rutuba kwa manufaa ya kilimo bora katika nchi yetu’’.
 
“Miti ni uchumi katika nchi, inatumika kujengea, kutengenezea samani za maofisini na majumbani, viwandani kutengeneza vitu mbalimbali ikiwamo viberiti na vyombo vya kusafiria vya baharini” alisema Makongoro.
 
Aidha, Makongoro alisema kuwa kutokana na hatari ya mabadiliko hali ya tabia nchi yanavyoendelea, ni wajibu wa kila Mtanzania kutunza mazingira na kuzingatia usemi wa “Kata mti, Panda miti” ili kuboresha hali ya hewa nchini na mazingira yawe rafiki kwa viumbe vyote vilivyopo kwenye maji na nchi kavu wakiwemo wanyama, mimea, samaki na viumbe wengine wanaoishi kwenye maji.
 
Katika tukio la upandaji miti, ilipandwa jumla ya miti mitatu katika taasisi ya TaSUBa ikiwa ni juhudi zinazofanywa na bunge la EALA katika kutunza mazingira kwa vitendo.
Mti wa pili ulipandwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara na wa tatu ulipandwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano ya Afrika Mashariki, Dkt. Abdala Juma Abdulla Saadalla.

No comments: