SERIKALI kupitia Wizara ya
Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, kwa kushirikiana na mashirika na
asasi anuai zinazotetea haki za watoto na jamii kwa ujumla imezinduwa
kampeni maalumu za kitaifa za kupinga ndoa za utotoni (National Ending
Child Marriage Campaign) ambazo zimekuwa zikikwamisha haki ya elimu kwa
mtoto wa kike.
Uzinduzi huo umefanyika leo jijini
Dar es Salaan kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi
ya Watu (UNFPA), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Shirika lisilo
la Kiserikali la Children’s Dignity Forum (CDF), Graca Machel Trust
(GMT), asasi za mkoani Mara na uongozi wa mkoa huo.
Akizungumza katika uzinduzi huo,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna
Maembe alisema Serikali ipo kwenye mchakato wa kupitia sheria zake
ikiwemo Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ambayo imekuwa na utata juu ya umri
wa kuolewa kwa mtoto wa kike. Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, pamoja na
mambo mengine inaruhusu mtoto wa kike miaka 14 au 15, kuolewa kwa ridhaa
ya wazazi au mahakama jambo ambalo linatajwa na wanaharakati kuwa
kikwazo cha elimu kwa mtoto huyo.
Akifafanua zaidi Katibu Mkuu
aliwahakikishia washiriki wa mkutano huo kuwa sheria hiyo itabadilika
hasa baada ya mchakato wa katiba kukamilika hivyo kuwataka wananchi kwa
kushirikiana na asasi anuai kuunga mkono juhudi za kupinga ndoa za
utotoni zinazoendekezwa kwa baadhi ya maeneo nchini Tanzania.
Alisema uwepo wa udhaifu wa sheria
isiwe kisingizio cha kuendeleza vitendo hivyo viovu kwenye jamii kwani
Serikali wakati wote kupitia watendaji wake ipo tayari kupambana na watu
wanaoendeleza vitendo hivyo pale inapofikishiwa taarifa.
“…Jamii lazima ikubali kubadilika
na kuacha vitendo hivi vya kuwaozesha watoto, hivi kati yetu hapa nani
anakubali mtoto wake akatishwe masomo na kuozeshwa? Tukiwa tayari kupiga
vita kuanzia kwenye familia zetu makazi yetu suala hili litakoma…Ni
kweli Serikali ipo kwenye utaratibu wa kuipitia sheria na nawahakikishia
itafanyiwa mabadiliko lakini kama jamii nasi tunatakiwa kubadilika na
kuacha vitendo hivi,” alisema Bi. Maembe.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa TAMWA, Valerie Nsoka alisema shughuli za kampeni hizo
maalumu za kupinga ndoa za utotoni zinatarajiwa kufanyika Mkoani Mara na
zitaambatana na utoaji elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi
wa dini, watendaji wa vyombo vinavyosimamia sheria, viongozi wa jamii na
jamii kwa ujumla juu ya mapambano ya kampeni hizo.
Alisema kampeni hizo baadaye
zitaendelea katika maeneo mengine ya Tanzania lakini kwa sasa Mkoa wa
Mara ndipo zitakapoanzia na limechukuliwa kama eneo la mfano kwa
kuanzia. “…Tunaamini tunaweza kushirikiana na jamii kwa kuwalinda watoto
wetu ambao wamekuwa wakinyimwa haki ya msingi ya kupata elimu na baadhi
ya watu,” alisema Bi. Nsoka.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Children’s Dignity Forum
(CDF), Koshuma Mtengeti akizungumza katika hafla hiyo alisema takwimu
zinaonesha Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo inaidadi kubwa ya ndoa
za utotoni. Aliongeza kuwa takwimu zinaonesha kati ya wasichana 5
wanaoolewa Tanzania wawili kati yao huolewa wakiwa chini ya miaka 18
ilhali sheria ikiendelea kuwa na utata.
Aidha Meneja wa Haki za Watoto
kutoka Graca Michel Trust, Bernard Orimbo juhudi za makusudi zikifanywa
kwa makundi yote kampeni hizo zinaweza kufanikiwa kwani taasisi hiyo kwa
kushirikiana na Serikali ya Zambia ilipata mafanikio makubwa dhidi ya
kampeni kama hizo zilizoanza kufanyika mwaka 2013.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment