Pages

KAPIPI TV

Wednesday, February 12, 2014

WANAWAKE 6200 KILA MWAKA WANAKUTWA NA UGONJWA WA SARATANI YA MLANGO WA UZAZI

IMG_9948Mara baada ya ufunguzi wa kampeni ya kutokomeza  saratani ya mlango wa kizazi, kutoka wa kwanza kushoto ni Rais wa taasisi ya Bristol Myer Squibb,Mkurugenzi mtendaji wa muungano wa utepe wa pinki na utepe mwekundu  Dr. Doyin Oluwole na anayefata ni Kaimu  Mkurugenzi wa huduma  za kinga toka wizara ya Afya Dr. Neema  Rusibamayilla. IMG_9969Wadau na washiriki  mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja  mara baada ya ya ufunguzi wa kampeni ya kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi iliyofanyika leo katika hoteli  ya Protea Courtyard jijini Dar es salaam. IMG_9911Rais wa taasisi ya  Bristol –Myers Squibb,John Damonti  akizungumza  wakat i wa  ufunguzi  wa  kampeni ya kutokomeza    ugonjwa wa saratani ya mlango  wa kizazi,ambao umekua aina  ya pili ya ugonjwa  wa saratani  inayokumba zaidi   wanawake waishio kusini na mashariki mwa Afrika baada ya Saratani ya IMG_9926Wadau na washiriki kutoka katika mashirika na taasisi mbalimbali wakifuatilia kwa makini wakati   ufunguzi wa kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa saratani ya kizazi uliyofanyika leo katika hoteli ya Protea Courtyard jijini Dar es salaam.
………………………………………………………………………………..
Na Anna Nkinda – Maelezo
 Tafiti zilizofanyika mwaka 2010 zinaonyesha kila mwaka wanawake 6200 wanakutwa na ugonjwa wa saratani  ya mlango wa kizazi  kati ya hao 4000 wanapoteza maisha  kwa kuwa  asilimia 10 ya wagonjwa hao wanaweza kuhudhuria Hospitali kwa ajili ya kupata huduma na matibabu.
Kutokana na utafiti huo Tanzania ni moja ya nchi yenye wagonjwa wengi wanausumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ukilinganisha na nchi nyingine zilizopo Afrika ya Mashariki.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Kinga kutoka wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Neema Rusibamayilla wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi ambayo inafadhiliwa na Muungano wa Utepe wa Pinki , Utepe mwekundu  wa nchini Marekani  uliofanyika leo katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.
Dk. Rusibamayilla alisema ugonjwa wa kansa ni tatizo hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania hii inatokana na sababu mbalimbali zinazozuia watu wasipate vipimo vya ugonjwa hii ikiwa ni pamoja na ukosekanaji wa taarifa za upimaji na utolewaji wa matibabu ya saratani, upatikanaji wa vifaa tiba, utoaji wa huduma, upungufu  wa watumishi wa huduma ya afya.
“Naamini mradi huu utaweza  kutatua baadhi ya changamoto zinazotukabili kama kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu  ugonjwa huu na upatikanaji wa vipimo  hii itasaidia kutatuwa tatizo mapema na kupunguza vifo  vya wanawake vinavyotokana na ugonjwa huu”, alisema Dk. Rusibamayilla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Utepe wa Pinki , Utepe Mwekundu  ambao unafanya kazi na Taasisi ya George W. Bush Dk. Doyin Oluwole aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa uongozi wake imara na kuamua kupambana na tatizo la ugonjwa wa saratani na hasa saratani zinazowasumbua wanawake.
Dk. Oluwole alisema, “Katika nchi zote tunazofanya kazi ikiwa ni pamoja na Tanzania malengo yetu ni kuimarisha miundombinu ya afya iliyopo na kufanya kazi na wadau wa afya na hakika tukiungana pamoja na kufanya kazi na watu wengi tutaweza kufika mbali zaidi.
Tuungane kuzuia saratani ya  mlango wa kizazi kwani wagonjwa wengi wa saratani ya shingo ya kizazi wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi”.
Alisema watafanya kazi na kuhakikisha wanafika nchi nzima hadi vijijini ili kuona  wanawake wanapata elimu , vipimo na matibabu na hivyo kuweza kuokoa maisha ya wanawake na wasichana ambao wanasumbuliwa na ugonjwa huo.
Kwa upande wake Dk. Serafina Mkuwa ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) alisema lengo la kuzinduliwa kwa mradi huo ni kuihamasisha jamii ili iweze kufanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.
“Tunatoa hamasa kwa wanawake na wasichana wasiogope bali waweze kujitokeza kwa wingi na kupima kwani ukipima na kutokutwa na tatizo  utafanyiwa tena uchunguzi baada ya miaka mitatu lakini ukipimwa na kukutwa na ugonjwa  unaanza matibabu na ugonjwa huu kama utaanza matibabu mapema utapona”, alisema Dk. Mkuwa.
 Naye Mkurugenzi wa Uboreshaji Afya kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Dk. Sara Maongezi alisema taasisi hiyo imepewa  jukumu la kuzungumza na viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali kuhusiana na ugonjwa huo.
“Tutaongea na kamati za Bunge za  Ukimwi na Ustawi wa jamii ili wakati wa kujadili bajeti ya wizara ya Afya waangaliea zaidi kuhusu saratani na katika ngazi ya mkoa  tutawakusanya wataalam wa afya kutoka mikoani na wilayani na kuwapa  elimu”, alisema Dk. Maongezi.
Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni maumivu makali chini ya kitovu, kutokwa na maji machafu ukeni, wakati wa kufanya  tendo la ndoa mwanamke atatokwa na damu na mwisho ni damu zinatoka zenyewe bila ya kufanya tendo la ndoa.
Mwezi wa saba mwaka 2013 Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa zamani wa Marekani ambaye pia ni mwanzilishi wa Taasisi ya  George W. Bush walizindua Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu (PRRR) nchini nia ikiwa ni kuzisaidia nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupunguza idadi ya wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya kizazi na matiti.
Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu ulitoa dola za Marekani milioni 1.2 fedha ambazo zitatumika katika mradi huo ambao kwa mara ya kwanza utaanza katika mikoa ya Mbeya, Mwanza na Iringa.
Kampeni hiyo inafanywa chini ya usimamizi wa wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na muungano wa Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu, Taasisi ya WAMA, MEWATA, T-MARC,TAYOWA na Mtandao wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi Mkoani Mbeya.

No comments: